Istanbul, Uturuki
Klabu ya Fenerbahce ya Uturuki na kocha wao Jose Mourinho wanajipanga kuwashitaki mahasimu wao Galatasaray kwa madai ya kushambulia na kuingilia haki binafsi za kocha huyo.
Galatasaray inamtuhumu Mourinho kwa kutoa kauli za ubaguzi wa rangi wakati wa mechi baina ya timu hizo mahasimu wakidai kwamba kauli ya kocha huyo si ya kiungwana.
Mourinho alinukuliwa akiwadhihaki waliokuwa kwenye benchi la timu ya Galatasaray siku ya mechi akidai kwamba walishangilia kwa kuruka kama nyani.
Fenerbahce walikana kauli hiyo kuwa na viashiria vyovyote vya kibaguzi badala yake ilitafsiriwa ndivyo sivyo na kupotosha maana iliyokusudiwa.
Taarifa ya klabu ya Fenerbahce iliyopatikana jana Ijumaa ilidai kwamba inakusudia kulifikisha suala hilo kwenye vyombo vya sheria na kudai fidia ya Dola 52,000.
Shirikisho la Soka Uturuki limemfungia Mourinho mechi nne na kumtoza faini ya Dola 44,00 kwa kauli aliyoitoa dhidi ya waamuzi wa soka nchini Uturuki.
Mourinho baada ya mechi dhidi ya Galatasaray, iliyochezeshwa na mwamuzi wa Slovenia, alisema anaunga mkono kutumiwa waamuzi wa kigeni kauli ambayo imetafsiriwa kuwa ni kuwadhihaki waamuzi wa Uturuki.
Wakati huo huo, kiungo wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya Ghana, Michael Essien ameibuka na kumtetea Mourinho katika tuhuma za ubaguzi wa rangi kama alivyofanya mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba.
Essien ambaye Mourinho aliwahi kuwa kocha wake katika klabu ya Chelsea alihusisha tuhuma zinazomkabili Mourinho na jambo baya la upotoshaji.
“Historia ya maisha yake kwa wakati wote amekuwa mtu mzuri kwa watu wote, duniani kote, na kwa watu wa mataifa tofauti, hilo liko wazi na linaeleweka,” alisema Essien.
Essien pia alisema kwamba kinachofanyika ni kujaribu kupotosha kauli ya Jose na mwisho watu wameona kitu kisicho sahihi na uwongo kutoka Galatasaray.