Zurich
Aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter yuko katika mbio za kulisafisha jina lake mahakamani kutokana na kashfa ya rushwa inayomuandama.
Katika kashfa ambayo bosi huyo wa zamani wa Fifa anapambana kujisafisha ni yale madai ya kwamba alitoa malipo yenye viashiria vya rushwa kwa mwanasoka wa zamani wa Ufaransa, Michel Platini.
Blatter ambaye amekuwa rais wa Fifa kwa miaka 17 kati ya mwaka 1998 hadi 2015, alisema kwamba yeye hajafanya kosa lolote badala yake amegeuzwa mlengwa wa michezo michafu.
Mwaka 2022, Blatter na Platini ambaye alikuwa rais Uefa wote walisafishwa na Mahakama Kuu Switzerland baada ya uchunguzi wa miaka saba uliohusisha malipo ya Dola 2.24 milioni ingawa uamuzi wa kuwasafisha umepingwa na kukatiwa rufaa na waendesha mashtaka wa Switzerland.
“
Mwaka 2022 Mahakama ya Jinai ilisema kwamba mkataba kati yangu na Platini ulikuwa halali na natarajia mahakama nyingine ingekubaliana na uamuzi huo, kukata rufaa ni upuuzi,” alisema Blatter.
Blatter ambaye kwa sasa ana miaka 88 alisisitiza kwamba anafanywa mlengwa wa michezo michafu na ni kama vile watu wamempania lakini ana uhakika atasafishwa kwani yeye ni mtu msafi.