Na mwandishi wetu
Simba na Azam FC zimetoka uwanjani kwa sare ya mabao 2-2 katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa leo Jumatatu, Februari 24, 2025 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Azam waliuanza mchezo kwa kasi na kufanya shambulizi katika dakika ya kwanza lililozaa bao mfungaji akiwa ni Gibril Sillah aliyeitumia pasi ya Idd Nado.
Mpira uliozaa bao ulitokana na makosa ya Fabrice Ngoma ambaye aliporwa mpira ukiwa katika miliki yake kabla ya kumkuta Sillah ambaye shuti lake la kwanza liliokolewa na kipa Mussa Camara kabla ya kumrudia mfungaji aliyeujaza wavuni.
Wakicheza kwa kujiamini Simba walianza kuliandama lango la Azam na kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Elly Mpanzu katika dakika ya 26.
Bao hilo lilitokana na juhudi za Kibu Denis ambaye aliinasa pasi ya Shomari Kapombe akiwa nje kidogo ya eneo la 18 la Simba, akaambaa na mpira na kuvuka kidogo eneo la kati ya uwanja kabla ya kumpasia Mpanzu.
Dakika ya 75 Simba waliandika bao la pili lililofungwa kwa kichwa na Abdulrazak Hamza akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Jean Ahoua, adhabu ambayo mwamuzi Ahmed Arajiga aliitoa baada ya Kibu kuchezewa rafu.
Matumaini ya Simba kutoka na pointi zote tatu yalizimwa na Zidane Sereri aliyeingia akitokea benchi katika dakika 10 za mwisho na kufunga bao la kusawazisha.
Bao hilo lilitokana na pasi ndefu ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ pasi ambayo haikutarajiwa kama ingemkuta mfungaji lakini ilitosha kuibua shangwe kwa mashabiki wa Azam.
Kwa matokeo hayo, Simba inaendelea kubaki nafasi ya pili ikiwa na pointi 51 katika mechi 20 wakiwa nyuma ya Yanga wanaoshika usukani wa ligi hiyo wakiwa na pointi 55 katika mechi 21.
Kimataifa Simba, Azam zatoka sare 2-2
Simba, Azam zatoka sare 2-2
Read also