Na mwandishi wetu
Timu ya soka ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars imeanza na mguu mzuri mbio za kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Wanawake (Wafcon) 2026 baada ya kuilamba Equatorial Guinea mabao 3-1.
Ushindi huo uliopatikana leo Alhamisi, Februari 20 kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi, Dar es Salaam unaibua matumaini makubwa kwa timu hiyo kufuzu fainali hizo.
Katika mechi hiyo walikuwa ni wageni Equatorial Guinea walioanza kwa kuzitikisa nyavu za Twiga dakika ya 42 kwa bao lililofungwa na Getruede Engueme na kuzifanya timu ziende mapumziko Twiga ikiwa nyuma kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili Twiga walianza kuonesha ubora wao na kufanikiwa kufunga mabao matatu la kwanza likifungwa na Stumai Abdallah dakika nne baada ya kuanza kipindi hicho.
Enekia Lunyamila aliongeza bao la pili kwa Twiga katika dakika ya 55 kabla Diana Msewa hajakamilisha bao la tatu dakika ya 90.
Baada ya ushindi huo, Twiga sasa inasubiri kurudiana na timu hiyo, Februari 26, mechi ambayo Twiga ikiwa ugenini itatakiwa kupata ushindi au hata sare ili kusonga mbele.
Kama mambo yatakwenda vizuri katika mechi ya marudiano, mechi inayofuata timu hiyo itaumana na mshindi wa mechi kati ya Ethiopia na Uganda.
Pamoja na matokeo hayo lakini Equatorial Guinea si timu ya kubeza katika soka la wanawake barani Afrika hasa ikikumbukwa kuwa mwaka 2012 ilibeba taji la Wafcon.
Kimataifa Twiga yailamba Equatorial Guinea 3-1
Twiga yailamba Equatorial Guinea 3-1
Read also