Madrid, Hispania
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti ameipotezea habari inayozidi kuvuma ya nyota wake, Vinicius Junior kuihama timu hiyo Majira ya Kiangazi na kwenda kucheza soka Saudi Arabia.
Kwa muda mrefu sasa Vinicius Jr au Vini amekuwa akihusishwa na mipango hiyo na habari zinadai kwamba katika mpango huo mchezaji huyo anatarajia kufanywa mchezaji anayelipwa fedha nyingi zaidi duniani.
Alipoulizwa Ancelotti hata hivyo alisema amechoshwa na habari hizo ingawa hazimpi wasiwasi wowote na wanachoona ni kwamba mchezaji huyo anafurahia maisha Real Madrid na wao wanamfurahia.
“Ndio nimechoshwa na habari hii lakini hainipi wasiwasi, namuona ni mwenye furaha hapa na sisi pia tunamfurahia, sina la kuongeza, hili si jambo ambalo tunalijadili hapa, hata Vinicius halijadili,” alisema Ancelotti.
Ancelotti alisema kuwa anachokiona kwa Viniius ni aina ya mchezaji mwenye furaha katika klabu hiyo na mwenye shauku ya kufanya mambo yake vizuri na kuweka historia akiwa na Real Madrid.
VinÃcius, 24, ambaye mkataba wake Real Madrid unafikia ukomo mwaka 2027, baada ya timu yake kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Man City Jumanne iliyopita katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, alisema anaamini hivi karibuni atafikia makubaliano ya kuongeza mkataba Real Madrid.
Habari ambazo si rasmi hata hivyo zinadai kwamba Vini ambaye yuko katika mwaka wake wa saba na Real Madrid, anachotaka ni kuona analipwa kumzidi Kylian Mbappe ambaye ndiye mchezaji anayelipwa zaidi katika klabu hiyo kwa sasa.
Vini anajivunia kuiwezesha Real Madrid kushinda mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na matatu ya La Liga, baada ya kushinda tuzo ya Fifa mwezi Desemba mwaka jana, klabu yake ilimuongezea marupurupu katika mshahara wake.