Mancheste, England
Kocha wa Man United, Ruben Amorim amesema klabu yao italazimika kuuza wachezaji kama watataka kununua mchezaji yeyote wakati wa dirisha kubwa la usajili Majira ya Kiangazi.
Mambo hayaendi vizuri kwa Man United katika Ligi Kuu England (EPL) msimu huu na upo uwezekano mkubwa wa timu hiyo kutoshiriki mashindano yoyote ya klabu barani Ulaya msimu ujao.
Hali hiyo hata hivyo haikuwafanya kujiimarisha kwa usajili mkubwa katika dirisha dogo la Januari badala yake walitumia Pauni 25 milioni tu kumsajili beki Patrick Dorgu.
Habari za ndani zinadai kwamba baada ya kupata hasara ya mamilioni ya Pauni katika miaka ya hivi karibuni, uimara wa klabu kuichumi unawalazimu kujibana katika matumizi.
Alipoulizwa kuhusu mpango wa kukiimarisha kikosi na suala zima la kubana matumizi, Amorim alisema kinachotakiwa kufanyika ni kuuza wachezaji ili kuweza kununua wengine.
Amorim hata hivyo alisisitiza kwamba wanachokiangalia kwa sasa ni namna ya kushinda mechi zilizo mbele yao na baada ya hapo akili yao itaanza kuangalia nini cha kufanya kwenye usajili.
Mpango mwingine uliopo katika klabu hiyo ni kuboresha timu za vijana ili kuwa na idadi ya kutosha ya wachezaji ambao baadaye watacheza kwenye kikosi cha kwanza au watauzwa badala ya kutegemea kununua wachezaji bei mbaya kutoka klabu nyingine.
Dalili njema zilizoanza kuonekana katika mpango huo ni kwenye kikosi cha Man United cha vijana chini ya miaka 18 ambacho Jumatano kilifuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la FA kwa vijana baada ya kuichapa Chelsea mabao 5-1.
Katika mechi hiyo nyota anayeonekana kuwa na kipaji Chido Obi alionesha uwezo wake baada ya kufunga mabao matatu (hat trick) peke yake.
Kimataifa Amorim: Lazima tuuze wachezaji
Amorim: Lazima tuuze wachezaji
Read also