Na mwandishi wetu
Simba imerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC baada ya kuinyuka Tanzania Prisons mabao 3-0 katika mechi iliyochezwa leo Jumanne, Februari 11, 2025 kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Ushindi wa Simba pia umekuwa faraja kubwa kwa nyota wao Ladack Chasambi ambaye amekuwa akisakamwa kwa siku kadhaa sasa baada ya kujifunga na kuifanya Simba itoke sare ya bao 1-1 na Fountain Gate na hivyo kushindwa kujiimarisha kileleni.
Chasambi leo amewasahaulisha yote hayo mashabiki wa Simba baada ya kufunga bao la tatu na la mwisho kwa timu yake katika mechi hiyo.
Baada ya matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 47 katika mechi 18 wakati mahasimu wao Yanga waliokuwa wanashikilia usukani wanashuka hadi nafasi ya pili wakiwa na pointi 46 katika mechi 18 kama za Simba.
Kiungo Jean Ahoua ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzitikisa nyavu za Prisons katika dakika ya 29 akiitumia vizuri pasi ya Shomari Kapombe, beki mwenye sifa ya kupanda na kutengeneza mashambulizi dhidi ya timu pinzani.
Dakika moja kabla ya timu kwenda mapumziko, Elly Mpanzu aliwainua vitini mashabiki wa Simba alipoandika bao la pili baada ya kuunganishiwa pasi na Leonel Ateba.
Wakati ikisubiriwa filimbi ya timu kwenda mapumziko dakika moja katika dakika za nyongeza ilitosha kuipatia Simba bao lililofungwa na Chasambi na kwa mara nyingine pasi ya Kapombe ambaye ndiye nyota wa mchezo wa leo, ikatumika kuzaa bao hilo.
Wakati matokeo hayo yakiipaisha Simba kileleni, kwa Prisons yanazidi kuwaweka pagumu kwa kuwa wanabaki na pointi zao 17 wakiwa nafasi ya 14 na hivyo wana kila sababu ya kupambana kujinasua na hatari ya kushuka daraja.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa leo, Mashujaa na Coastal Union zilitoka sare ya 0-0 wakati Kagera Sugar na Tabora United.
Soka Simba yarudi kileleni
Simba yarudi kileleni
Read also