Manchester, England
Baada ya kushinda mechi ya raundi ya nne ya Kombe la FA dhidi ya Leyton Orient, kocha wa Man City, Pep Guardiola amewadhihaki mashabiki akidai ushindi huo umeokoa kibarua chake.
Man City nusura iadhirike mbele ya timu hiyo ya Ligi One baada ya kwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 1-0 na ndipo mashabiki wa Orient walipoanza kumzomea Pep kwa kumwambia anafukuzwa kazi.
Mabao ya kipindi cha pili ya Abdukodir Khusanov na Kevin de Bruyne yalitosha kumpa ushindi wa 2-1 na hivyo kumnusuru Pep kuadhirika kwa mara nyingine wakati huu timu yake ikiandamwa na matokeo mabaya hasa kwenye Ligi Kuu England (EPL).
Pep hata hivyo alipoulizwa baada ya mechi hiyo kuhusu ushangiliaji wa mashabiki wa timu pinzani kama aliufurahia alisema hakufurahia kwa sana hasa walipokuwa wakisema anafutwa kazi kesho.
“Ni mwendelezo wa matukio katika viwanja vyote kwa sasa, lakini kwa matokeo haya nafikiri mwenyekiti wangu hatonifukuza kazi kesho (Jumapili),” alisema Pep.
Pep hata hivyo alisema kwamba kimsingi hali hiyoya ushangiliaji ni nzuri ingawa hajui kama ni kwa kila mechi ya Ligi One hamasa ni ya aina hiyo na kwa ujumla hilo si jambo baya.
Man City watakuwa na kibarua kigumu keshokutwa Jumanne watakapoumana na Real Madrid katika mechi ya kwanza ya hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Akizungumzia matokeo mabaya ya timu yake, Pep alisema kwa wakati huu hawako sawa wana janga la wachezaji wengi majeruhi na hivyo wanapopata ushindi anajiona mwenye furaha na kujivunia matokeo.