Manchester, England
Kocha wa Man United, Ruben Amorim amesema uamuzi wa kutosajili wachezaji zaidi katika dirisha dogo la Januari ni wake licha ya kwamba utawaweka katika mazingira magumu.
Hadi dirisha dogo la usajili linafungwa mapema wiki hii, Man United imefanya usajili wa wachezaji wiwili tu, beki wa kushoto Patrick Dorgu, 20, kutoka Lecce ya Italia na beki wa kati Ayden Heaven, 18, kutoka Arsenal.
Baada ya kumtoa kwa mkopo Marcus RAshford aliyejiunga na Aston Villa na kumruhusu Antony kujiunga na Real Betis, ilitarajiwa timu hiyo pia ingejiimarisha kwa kusajili japo mshambuliaji mmoja.
Amorim hata hivyo baada ya dirisha la usajili kufungwa alisema kwamba walifanya kila wawezalo ili kuimarisha kikosi kwa kusajili zaidi lakini wameshindwa kuongeza wachezaji wengine.
“Tumechukua uamuzi mgumu lakini ni kwa sababu tunahitaji kitu tofauti katika timu, hadhi na sifa tofauti, ulikuwa ni uamuzi wangu kufanya hivyo,” alisema Amorim.
Kocha huyo alifafanua kwamba anachokiona ni kuwa klabu inajipa muda ingawa wanajua mahitaji ya wakati huu ya timu lakini hakuna anayetaka kufanya makosa ya siku za nyuma.
“Katika kipindi cha usajili majira ya kiangazi tutaona itakavyokuwa, lakini kama nilivyosema kwa hakika tunakuwa makini katika usajili kwa sababu kuna makosa tuliyofanya siku za nyuma,” alisema Amorim.
Keshokutwa Ijumaa, Man United itaumana na Leicester City kwenye dimba la nyumbani Old Trafford katika mechi ya raundi ya nne ya Kombe la FA, mechi ambayo huenda wachezaji wapya, Dorgu na Heaven watapata nafasi ya kuiwakilisha timu yao mpya kwa mara ya kwanza.