London, England
Beki wa zamani wa Man United, Gary Neville amemshutumu beki wa Arsenal, Gabriel kwa kumdhihaki Erling Haaland katika mechi ya jana Jumapili ambayo Arsenal iliichapa Man City mabao 5-1.
Gabriel mara baada ya Martin Ødegaard kufunga bao la kuongoza la Arsenal, akiwa karibu kabisa na Haaland alifanya kama kumkoromea usoni kama namna mojawapo ya kumdhihaki na kushangilia bao hilo.
Baada ya Myles Lewis-Skelly kufunga bao jingine, mchezaji huyo alifanya dhihaka kwa kujifanya kama anashangilia kwa staili ya Haaland.
Tukio hilo limetokea huku kukiwa na kumbukumbu ya mechi baina ya Man City na Arsenal iliyochezwa Septemba mwaka jana ambapo Haaland alimpiga Gabriel na mpira kichwani kwa nyuma.
Tukio hilo lilisababisha mzozo kati ya Haaland na baadhi ya wachezaji wa Arsenal baada ya mwamuzi kupuliza filimbi ya kumalizika mchezo.
Akizungumzia tukio hilo, Neville alisema kwamba lilimnyima raha na lilikuwa ni la kukosa heshima kwa beki huyo wa kati.
Neville alisema tukio kama hilo liliwahi kumtokea miaka mingi iliyopita kwenye dimba la Highbury ingawa mwishowe walitoka na ushindi wa mabao 4-2 lakini kuna mchezaji alimfuata na kumkoromea usoni.
“Kwa hakika sikupenda, nadhani ni tukio la kukosa heshima, nimeliona hilo kwa Haaland, kuna kitu ambacho sikukipenda, sikuwahi kwenda kumkoromea mchezaji usoni, sikupenda jambo hilo, ni namna fulani ya kukosa heshima,” alisema Neville.
Baada ya tukio hilo, kocha wa Arsenal, Mikel Arteta alionekana kuwaonya wachezaji wake kuhusu kushangilia kwa kumdhihaki moja kwa moja Haaland.
Arsenal ipo nyuma ya vinara wa Ligi Kuu England (EPL) Liverpool kwa tofauti ya pointi sita na Liverpool wapo nyuma kwa mechi moja ambayo wataicheza keshokutwa Jumatano dhidi ya Everton.