Na mwandishi wetu
Simba imetoa kipigo cha mabao 6-0 kwa Kilimanjaro Wonders katika mechi ya Kombe la TFF iliyopigwa leo Jumapili Januari, 25, 2025 kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge, Dar es Salaam.
Simba ilitawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa na haikushangaza kupata ushindi huo mnono ambao umewawezesha kufuzu hatua ya 32 bora ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Benki ya CRDB.
Timu hiyo iliandika bao lake la kwanza mapema sekunde ya 18 lililofungwa na Valentino Mashaka akiitumia vizuri krosi ya beki Valentine Nouma.
Dakika mbili baadaye, Simba waliongeza bao la pili mfungaji akiwa ni Ladak Chasambi ambaye aliitumia pasi ya David Kameta ‘Duchu’.
Mashambulizi ya Simba yalizidi kuwaweka pagumu vijana wa Wonders ambao dakika ya 10 waliizawadia Simba bao la tatu baada ya Patrick Sebastian kujifunga wakati akiokoa mpira uliopigwa na Nouma.
Simba waliendelea kuwanyanyasa Kili Wonders na kuandika bao la nne lililofungwa na Joshua Mutale na hivyo kwenda mapumziko huku ubao ukisoma 4-0.
Mabao mengine mawili ya Simba yalipatikana kipindi cha pili wafungaji wakiwa ni Steven Mukwala aliyefunga bao la tano kwa kichwa wakati lile la sita lilifungwa Edwin Balua.
Simba ambayo golini ilimuweka kipa Ally Salim ambaye hakupata kashkasha za mara kwa mara kwani mashambulizi pekee ya kushtua ya Wonders yalifanywa dakika ya 9 na 10 ya kipindi cha pili.
Kwa ushindi huo Simba inakuwa imefuzu hatua ya 32 bora ya michuano hiyo ambayo pia inajulikana kwa jina la CRDB Federation Cup.
Kimataifa Simba yaipa Wonders dozi ya 6-0
Simba yaipa Wonders dozi ya 6-0
Read also