Na mwandishi wetu
Baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga imehamishia hasira zake kwenye Kombe la TFF baada ya kuilaza Copco United ya Mwanza mabao 5-0.
Matokeo ya mechi hiyo iliyopigwa leo Jumamosi, Januari 25, 2025 kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge, Dar es Salaam yanaifanya Yanga kufuzu hatua ya 32 bora ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Benki ya CRDB.
Shekhan Ibrahim ndiye aliyekuwa wa kwanza kufungua ukurasa wa mabao kwa Yanga dakika ya 35 baada ya kuandika bao kwa kichwa akitumia mpira wa kona iliyochongwa na Farid Mussa.
Copco walijitahidi kuwadhibiti Yanga kwa kipindi chote cha kwanza kabla mambo hayajawa mabaya dakika 13 baada ya kuanza kipindi cha pili walipofungwa bao la pili mfungaji akiwa Prince Dube kwa pasi ya Israel Mwenda.
Majanga yaliendelea kuisakama Copco katika dakika ya 68 walipopachikwa bao la tatu mfungaji akiwa ni Maxi Nzengeli kwa mkwaju wa penalti.
Duke Abuya aliipatia Yanga bao la nne dakika ya 78 akitumia krosi ya Nickson Kibabage wakati karamu ya mabao ilihitimishwa na Mudathir Yahya kwa bao la kichwa lililotokana na krosi ya Israel Mwenda.
Timu nyingine ambazo zimefuzu hatua hiyo pamoja na Yanga ni Cosmopolitan, JKT Tanzania, Mbeya City, Green Warriors, TMA Stars, Namungo FC na Polisi Tanzania.
Nyingine ni Coastal Union, KMC, Pamba Jiji, Town Stars, Stand United, Fountain Gate, Leo Tena, Azam FC, Kiluvya United na Songea United,
Katika orodha hiyo pia zimo, Prisons, Big Man FC, Tabora United, Mashujaa FC, Singida Black Stars, Transit Camp, Biashara United, Mtibwa Sugar, Mambali FC, Kagera Sugar, Geita Gold, Giraffe Academy na Mbeya Kwanza.
Timu nyingine zinazowania nafasi hiyo ni Simba na Kilimanjaro Wonders ambazo zitaumana kesho Jumapili Januari 26 ambapo moja kati ya hizo itafuzu hatua hiyo.
Soka Yanga yaipiga tano Copco United
Yanga yaipiga tano Copco United
Read also