Riyadh, Saudi Arabia
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil, Neymar Jr amesema nyota mwenzake waliyecheza pamoja PSG, Kylian Mbappé alikuwa mwenye wivu baada ya Lionel Messi kusajiliwa timu hiyo.
Neymar ambaye kwa sasa anaichezea Al Hilal ya Saudi Arabia na Mbappe ambaye kwa sasa anaichezea Real Madrid wamewahi kuwa pamoja PSG na Messi ambaye kwa sasa anacheza soka nchini Marekani.
Akifafanua kuhusu hilo, Neymar ambaye amekuwa akiandamwa na tatizo la kuwa majeruhi tangu kujiunga na Al Hilal, alisema wivu wa Mbappe uliathiri kiwango cha timu ya PSG.
Neymar alikuwa akijibu swali aliloulizwa na nyota wa zamani wa Brazil, Romario ambaye alitaka kujua iwapo Mbappe hakufurahia uwapo wa Messi katika timu ya PSG.
“Hapana hakufurahia, nilikuwa na mambo kadha wa kadha na yeye, ugomvi wa hapa na pale lakini alikuwa mtu muhimu tulipowasili pale, nilikuwa nikimwita kwa jina la golden boy,” alisema Neymar.
Neymar aliongeza kwa kusema kuwa wakati wote alikuwa akicheza pamoja na Mbappe, na kumwambia kwamba atakuja kuwa mmoja wa wachezaji bora, alimsaidia na kuzungumza naye na kuna siku walikuwa wakila pamoja chakula cha jioni nyumbani kwa Neymar.
“Tulikuwa na miaka mizuri ya ushirikiano, lakini Messi alipojiunga na timu kidogo akawa na wivu, hakutaka mimi niwe karibu na mtu mwingine, na hapo kukawa na ugomvi na kubadilika kwa tabia,” alisema Neymar.
Neymar alisema si vibaya kuwa na wivu kidogo na kila mahali kuna wivu lakini ni lazima kufahamu kwamba uwanjani huchezi peke yako anahitajika mtu mwingine wa kusaidiana na wewe na huwezi kushinda chochote bila ya kusaidiana na wenzako.
Mbappé alijiunga na PSG mwaka 2017 akitokea Monaco, mwaka ambao Neymar alijiunga na timu hiyo akitokea Barcelona ukiwa ni mmoja wa usajili uliokuwa gumzo katika historia ya soka wakati Messi alijiunga na PSG mwaka 2021 akiwa mchezaji huru.