Na mwandishi wetu
Yanga imepiga hatua muhimu kuelekea kufuzu robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuilaza Al Hilal ya Sudan bao 1-0 mechi iliyopigwa Jumapili hii usiku nchini Mauritania.
Bao hilo peke lililofungwa na Stephane Aziz Ki mapema dakika ya saba linaifanya Yanga kufikisha pointi saba na sasa italazimika kushinda mechi ijayo dhidi ya MC Alger ili kujikatia tiketi ya robo fainali.
MC Alger yenye pointi nane nayo inapigania nafasi hiyo jambo ambalo linaifanya mechi hiyo itakayopigwa Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kuwa ngumu kwa timu zote.
Aziz Ki anayesifika kwa kufunga mabao ya mashuti ya mbali, alifunga bao hilo baada ya kuinasa pasi ya chinichini aliyopenyezewa na Dickson Job.
Baada ya kuinasa pasi hiyo, Aziz Ki aliambaa kidogo na mpira kabla ya kuuweka sawa kwenye mguu wake wa kushoto na kufumua shuti lililomshinda mlinda mlango wa Al Hilal, Issa Fofana.
Yanga ilikuwa na nafasi ya kuongeza bao la pili katika dakika ya 44 baada ya Aziz Ki kuuwahi mpira uliopigwa vibaya na beki wa Sudan lakini shuti la Aziz Ki lilipaa juu ya lango.
Dakika ya 76, Prince Dube aliunasa mpira akiwa karibu na lango la Al Hilal wakati kipa wa timu hiyo akiwa ametoka lakini Dube akapiga mpira uliookolewa kirahisi.
Kimataifa Yanga yanusa robo fainali Afrika
Yanga yanusa robo fainali Afrika
Read also