London, England
Kocha David Moyes hatimaye ameteuliwa rasmi kuinoa Everton baada ya kuhusishwa na timu hiyo ambayo hivi karibuni ilimfuta kazi kocha Sean Dyche.
Moyes, 61, amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu na amefurahia hatua ya klabu hiyo kumrudisha kwa mara nyingine akisema kwamba kwake hilo ni jambo kubwa.
Kocha huyo hata hivyo anaichukua timu hiyo ikiwa inapitia kipindi kigumu kwenye Ligi Kuu England, inashika nafasi ya 16 baada ya kucheza mechi 19 na ni kati ya timu zenye hatihati ya kushuka daraja.
“Niliifurahia miaka 11 ya kipekee na yenye mafanikio na Everton na sikusita nilipopewa nafasi ya kurudi kwa mara nyingine katika klabu hii kubwa,” alisema Moyes
Alisema kinachotakiwa kwa sasa ni watu wote wa Everton kutoa mchango wao kwa kuwa karibu na wachezaji katika msimu huu muhimu ili watakapohamia kwenye uwanja wao mpya wawe ni timu ya ligi kuu.
Moyes alikuwa kocha wa Everton kuanzia mwaka 2002 hadi 2013 alipojiunga na Man United kuchukua nafasi iliyoachwa na kocha wa muda mrefu wa timu hiyo, Sir Alex Ferguson.
Mambo hata hivyo hayakwenda vizuri Man United na kujikuta akitimuliwa na baada ya hapo, Moyes alizinoa timu za Real Sociedad, Sunderland na West Ham aliyoinoa mara mbili.
Akiwa West Ham anaendelea kukumbukwa kwa kuiwezesha timu hiyo kubeba taji la Europa Conference Ligi mwaka 2023 na tangu atoke West Ham amekuwa bila ya timu.