Na mwandishi wetu
Aliyekuwa meneja habari na mawasiliano wa Yanga, Haji Manara amelazimika kuomba radhi baada ya kuonesha ukaidi na kumjibu jeuri ofisa mmoja wa Jeshi la Magereza.
Tukio hilo lilitokea Jumapili wakati wa mechi ya Yanga na Prisons kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam, mechi ambayo iliisha kwa Yanga kutoka uwanjani na ushindi wa mabao 4-0.
Manara akiwa nje ya uwanja huo kwa mahojiano na waandishi wa habari, ofisa huyo alitoa amri ya kumtaka aondoke eneo hilo karibu na gari inayodhaniwa kuwa ya magereza lakini Manara alipingana na ofisa huyo.
Akionekana mwenye kujiamini, Manara alikaidi agizo hilo ambapo alisikika akimhoji ofisa huyo kwa kuuliza, “huyu jamaa anasema nini? sauti ye pembeni ikasikika ikimjibu hilo ni gari lao, tuendelee.”
Ofisa huyo alishikilia msimamo wa kuwataka waondoke na ndipo Manara alipomwambia wewe nani mpaka unatoa amri na kumwambia kwamba hawezi kutoa amri.
“Yaani kwa sababu wewe ofisa magereza, watolee amri wafungwa wenzio sio mimi, tena nilikuwa sitaki kuondoka aya utafanya nini, lete askari wenzio, unataka kuntisha mimi,” Alihoji Manara.
Tukio hilo lilisababisha Jeshi la Magereza kutoa tamko jana Jumatatu, tamko ambalo lilisainiwana na msemaji wa jeshi hilo, Elizabeth Mbezi.
Katika tamko hilo jeshi hilo lilieleza tukio lilivyokuwa na jinsi Manara alivyotakiwa kuondoa gari lake ili gari jingine liweze kupita lakini akakaidi kwa dharau.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kauli ya Manara imetajwa kuwa ni kauli isiyo ya kiungwana, yenye viashiria vya kutweza utu na yenye mwelekeo wa kulifedhehesha Jeshi la Magereza.
Jeshi hilo kupitia taarifa hiyo pia limewaonya wananchi kuacha kutoa kauli zenye mwelekeo wa kubeza, kutweza na kudharau mamlaka ya jeshi hilo.
Baada ya taarifa hiyo, Manara naye Jumatatu hiyo hiyo akaibuka na taarifa ya kuomba radhi ambayo imepatikana kwenye mitandao ya kijamii.
Katika taarifa hiyo Manara anasema, “Watanzania, mashabiki wa mpira na wote ambao mtabahatika kuisikiliza video hii ambayo nimeamua kuitoa baada ya kuona kuanzia jana (Jumapili) kwenye social media kuna clip ambayo inatembea bahati mbaya sana imekwua edited (imehaririwa) na haijakamilika,” alisema Manara.
“Lakini kabla ya yote ni vizuri nikatanguliza neno kubwa na zito la samahani kwa yeyote ambaye amekwazika kwa namna moja ama nyingine kutokana na video ile hususan Jeshi la Magereza na yeyote yule ambaye amekwazika na kile alichokiona kwenye mitandao ya kijamii,” alisema Manara.
“Sikuwa na nia ya kusema chochote lakini hapa kuna issue ya taasisi ya Magereza na issue ya kibinadamu nikaona bora nitoe maelezo,” alisema Manara.