Manchester, England
Mshambuliaji wa Man United, Marcus Rashford amesema yupo tayari kwa changamoto mpya nje ya klabu hiyo baada ya kuwapo habari kwamba hali si shwari kati yake na kocha Ruben Amorim.
Rashford, 27 aliwekwa kando kwenye kikosi cha timu hiyo kilichocheza Jumapili na mahasimu wao wa jiji la Manchester, Man City na kutoka na ushindi wa mabao 2-1.
Kwa upande wako kocha Amorim amesema japo aliamua kumuweka kando Rashford katika mechi dhidi ya Man City lakini hakuna tatizo lolote la kinidhamu kwa mchezaji huyo.
Amorim hata hivyo anakumbukwa kwa kauli yake ya awali akidai kwamba anatarajia makubwa zaidi kwa nyota huyo wa England kwa mambo ya uwanjani na hata yale ya nje ya uwanja.
Habari ambayo imepatikana katika mtandao wa X au Twitter, mchezaji huyo amesema kwamba iwapo atafahamu kwamba hali imekuwa mbaya kwake hatopenda kuona inakuwa mbaya zaidi.
Rashford amefafanua kuwa ameshuhudia wachezaji kadhaa siku za nyuma namna wanavyoondoka katika klabu hiyo na yeye asingependa ajikute katika hali kama hiyo.
“Nitakapotaka kuondoka nitatoa taarifa na itakuwa taarifa kutoka kwangu, sitokuwa na kinyongo na yeyote, sitokuwa na kauli mbaya kuhusu Manchester United, huyo ndiye mimi,” alisema Rashford.
Rashford aliyeibukia timu ya vijana ya Man United kabla ya kuanza kucheza kikosi cha kwanza mwaka 2016, alisema kwa namna anavyojiona anadhani yuko tayari kwa changamoto mpya na hatua nyingine.
Nyota ya mshambuliaji huyo iling’ara katika msimu wa 2022-23 alipofunga mabao 30 katika mashindano yote lakini baada ya msimu huo ubora wake umekuwa wa kupanda na kushuka hali ambayo imemfanya ajikute akilaumiwa mara kwa mara.
Kitendo cha Amorim kutomjumuisha katika mechi na Man City kimezidi kuibua utata juu ya majaliwa ya mchezaji huyo na kocha huyo alipoulizwa hakuwa na jibu la moja kwa moja.
“Ni muhimu kusema kwamba halikuwa suala la kinidhamu, wiki ijayo, mechi ijayo, maisha mapya na wachezaji wanapigania nafasi, kwangu la muhimu ni kiwango bora mazoezini, kiwango bora kwenye mechi, namna unavyovaa, unavyokula, unavyojihusisha na wenzako na namna unavyoipeeka timu mbele,” alisema Amorim.
Nidhamu ya Rashford iliwahi kujadiliwa na nahodha wa zamani wa Man United, Gary Neville baada ya mchezaji huyo kwenda Marekani wakati wa mapumziko ya hivi karibuni kupisha mechi za kimataifa.
Neville ambaye ni mchambuzi wa soka hakupendezwa na kitendo hicho hasa baada ya mchezaji huyo kuonekana akishuhudia mechi za mpira wa kikapu za NBA jijini New York.
Kwa upande wake Rashford akizungumzia kitendo cha kuachwa katika mechi dhidi ya Man City alisema, Inaumiza moyo kuachwa kwenye derby lakini hayo hutokea na walishinda mechi hivyo muhimu kuangalia mbele.
“Inakatisha tamaa lakini mimi nimeshakuwa mtu mzima na naweza kukabiliana na hali ya kukatishwa tamaa, lakini pia nifanye nini? Nijikalie na kuanza kulia? Au nifanye bidii wakati mwingine nikipewa nafasi?” Alihoji Rshford.
Rashford pia alielezea kufurahishwa kwake na hatua ya kurudishwa kwenye kikosi cha England na kocha mpya Thomas Tuchel baada ya kuachwa na Gareth Southgate kwenye kikosi kilichoshiriki fainali za Euro 2024 nchini Ujerumani na kutolewa kwenye fainali na Hispania waliobeba taji.