Na mwandishi wetu
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetoa angalizo kwa mawakala wa soka nchini na kubainisha kuwa wanaotambulika ni wale tu wenye leseni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Taarifa ya TFF iliyopatikana Jumanne hii na kusainiwa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa shirikisho hilo, Cliford Ndimbo (pichani) ilitoa tahadhari kuwa mbele ya kamati zake haitotambua uwakilishi wowote wa wakala asiye na leseni.
“TFF haitotambua uwakilishi wowote kwa mchezaji ikiwamo uhamisho na mashauri mengineyo kwa wakala ambaye hana leseni ya Fifa,” ilifafanua taarifa hiyo.
Ndimbo ameibainisha kuwa kwa mujibu wa kanuni za Fifa ni wakala wa shirikisho hilo pekee ambaye anaweza kufanya shughuli za uwakala katika mchezo wa soka.
Tarifa hiyo pia imewataka wanaotaka kufanya shughuli za uwakala kuhakikisha wanafanya mtihani wa uwakala na kufaulu ili wapewe leseni na Fifa. Mtihani wa uwakala wa Fifa hufanyika mara mbili kwa mwaka.
TFF pia imetoa onyo kwa yeyote anayefanya shughuli za uwakala katika soka bila ya kuwa na leseni kuwa shirikisho hilo halitosita kupeleka taarifa za mtu huyo Fifa ili achukuliwe hatua.
Hadi sasa Tanzania ina mawakala wa soka saba tu wanaotambuliwa na Fifa ambao ni Ismail Hassan, Nassir Mjandari, Latifa Idd Pagal, Eliya Samwel Rioba, Benjamin Masige, Erick Mavike na Hadji Shaaban Omar.
Soka TFF yawanyooshea kidole mawakala
TFF yawanyooshea kidole mawakala
Read also