Manchester, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola amepuuza habari kwamba ana ugomvi na kiungo, Kevin de Bruyne badala yake amesema ana shauku kubwa kumuona nyota huyo akirejea katika ubora wake.
Kiungo huyo mahiri amekuwa akiandamwa na janga la kuwa majeruhi na amecheza kuanzia kipindi cha kwanza katika mechi nne tu za Ligi Kuu England (EPL).
Kwa ujumla De Bruyne amecheza dakika 72 zikiwamo mechi tano ambazo ameingizwa akitokea benchi tangu kuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya wiki nane kutokana na kuandamwa na majanga ya kuwa majeruhi.
Katika mechi ya Man City na Liverpool iliyopigwa Jumapili na City kulala kwa mabao 2-0, De Bruyne aliingia dakika 12 za mwisho na kufanikiwa kutengeneza nafasi ambayo bado kidogo iipatie City bao.
Wachambuzi wawili wa soka ambao pia ni wanasoka wa zamani Jamie Carragher na Gary Neville wote wamehoji namna Pep anavyompa nafasi De Bruyne na kujiaminisha kwamba kuna tatizo baina ya wawili hao.
Katika kilichoonekana kama kujibu hoja hizo bila kuwataja majina, Pep amesema kwamba hakuna jambo lolote baya kati yake na De Bruyne.
“Kuna wanaosema kuna tatizo kati yangu na Kevin, mnadhani sitaki kumchezesha, sitaki Kevin acheze? Mtu ambaye ana kipaji, sikihitaji hicho kipaji, eti nina tatizo binafsi naye baada ya miaka tisa?” Alihoji Pep.
Pep alifafanua kwamba mchezaji huyo amempa mafanikio makubwa kwenye klabu ya Man City na ana shauku kubwa ya kumuona akirudi katika ubora wake.
“Lakini huyu amekuwa nje kwa miezi mitano akiwa majeruhi, na akaumia tena na kuwa nje kwa miezi miwili, ana miaka 33, anahitaji muda arudi katika ubora wake,” alisema Pep.
Mkataba wa De Bruyne na Man City utafikia ukomo Juni mwakani na mchezaji huyo amethibitisha kuwa hakuna mazungumzo yaliyofanyika hadi sasa kuhusu kumuongezea mkataba ingawa kwa sasa anachokipigania ni kurudi katika kiwango chake bora.