Conakry, Guinea
Mashabiki 56 wa soka nchini Guinea wamefariki na wengine mamia kujeruhiwa baada ya vurugu kuibuka kwenye kwenye mechi chanzo kikiwa ni baadhi ya mashabiki kutoridhishwa na maamuzi.
Tukio hilo lilitokea Jumapili kwenye Uwanja wa 3 Avril uliopo kusini mwa Guinea wakati wa mechi maalum ya heshima ya kiongozi wa taifa hilo, Mamady Doumbouya.
Mechi hiyo ilihusisha timu za Nzerekore waliokuwa wenyeji dhidi ya Labe ambapo maelfu ya mashabiki walijazana uwanjani wakiwamo watoto ambao nao wanadaiwa kuathiriwa na tukio hilo.
Vurugu ziliibuka katika dakika ya 82 ya mchezo huo baada ya mwamuzi kumpa kadi nyekundu mchezaji mmoja wa Labe pamoja na kuipa timu pinzani penalti.
Kitendo hicho kilionekana kuwakera baadhi ya mashabiki wa Labe ambao walivamia uwanja na kuanza kurusha mawe jambo lililowafanya maofisa usalama waliokuwa uwanjani kujibu mapigo kwa kufyatua mabomu ya machozi.
Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya mashabiki kuanza kukimbia kwa lengo la kujiokoa na ndipo baadhi yao walipokanyagwa na kuumizana na wengine kujikuta wakipoteza maisha.
Waziri Mkuu wa Guinea, Bah Oury katika taarifa yake kupitia mtandao wa Twitter au X alilaani tukio hilo na kuomba utulivu akisema serikali itatoa taarifa baada ya kufanyia uchunguzi kiini cha tukio hilo.
Kwa upande wake rais wa zamani wa nchi hiyo, Alpha Condé katika taarifa yake alitoa shutuma akielezea kukosekana kwa uwajibikaji katika nchi hiyo katika kipindi hicho ambapo nchi hiyo inakabiliwa na majanga na vikwazo.
Hili si tukio la kwanza la vifo kwenye viwanja vya soka nchini Guinea, mwaka 2009, watu 150 walifariki na wengine kujeruhiwa ikiwamo kubakwa kwa wanawake baada ya waandamanaji wanaokadiriwa kufikia 50,000 kuandamana wakipinga mpango wa aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo, Dadis Camara kuwania urais katika uchaguzi wa kidemokrasia.
Chama kimoja cha upinzani nchini humo kimetaka uchunguzi ufanyike kwa madai kwamba mechi hiyo iliandaliwa kwa lengo la kumfanyia kampeni Doumbouya katika harakati zake za kujijenga kisiasa.
Doumbouya ambaye ni kiongozi wa kijeshi aliingia madarakani mwaka 2021 baada ya mapinduzi yaliyoutoa madarakani utawala wa kidemokrasia wa Conde na Oktoba mwaka jana alivifuta vyama 53 vya kisiasa.
Kimataifa Mashabiki 56 wafariki uwanjani Guinea
Mashabiki 56 wafariki uwanjani Guinea
Related posts
Read also