Munich, Ujerumani
Mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Kane huenda akaikosa mechi ya Jumanne hii ya Kombe la Ujerumani dhidi ya mabingwa watetezi Bayer Leverkusen baada ya kuumia katika mechi dhidi ya Borussia Dortmund.
Kocha wa Bayern, Vincent Kompany aliyasema hayo baada ya mechi hiyo iliyopigwa Jumamosi hii jioni na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Kane ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya England alitoka uwanjani dakika ya 33 wakati huo Dortmund wakiwa mbele kwa bao 1-0 kabla ya Bayern kusawazisha dakika ya 85 kwa bao la Jamal Musiala.
Kompany hata hivyo alisema kwamba tatizo la Kane huenda lisiwe kubwa lakini watalazimika kusubiri kwa kuwa mchezaji huyo atafanyiwa vipimo na hapo ndipo ukubwa wa tatizo utakapojulikana.
“Hata hivyo hali itakuwa ngumu kwa Jumanne bado sijaweza kuwajua wachezaji wengi ambao wana uwezo wa kupona kwa haraka katika muda mfupi namna hiyo,” alisema Kompany.
Kompany alikiri kwamba umahiri wa Kane katika upachikaji mabao unawapa ugumu wa kumpata mbadala wa kuziba pengo lake ingawa alisisitiza kwamba tangu mwanzo wa msimu wamekuwa wakikiamini kikosi chao.
“Huwezi kupata mchezaji wa kiwango chake kuziba pengo lakini vijana wana uwezo wa kufanya mambo kwa pamoja,” alisema Kompany.
Kabla ya mechi na Dortmund, Bayern walishinda mechi saba zilizopita za mashindano yote bila ya kufungwa hata bao moja na mechi yao ya kesho Jumanne dhidi ya Leverkusen inatajwa kuwa mtihani mgumu kwa timu hiyo.
Kimataifa Majeruhi Kane kuwakosa Leverkusen
Majeruhi Kane kuwakosa Leverkusen
Read also