Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imefuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 zitakazofanyika nchini Morocco baada ya kuilaza Guinea bao 1-0.
Ushindi huo umepatikana Jumanne hii Novemba 19, 2024 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kwa bao hilo pekee lililofungwa na Simon Msuva.
Bao hilo limetosha kuifanya Stars iweke rekodi ya kufuzu fainali hizo zinazoshirikisha nchi za Mataifa ya Afrika kwa mara ya nne kuanzia mwaka 1980, 2018 na 2023.
Msuva alifunga bao hilo dakika ya 60 akimalizia pasi ya juu ya Mudathir Yahya na kuruka kabla ya kuupiga mpira wa kichwa ambao ulimshinda kipa wa Guinea, Mussa Camara ambaye pia anaidakis timu ya Simba.
Ushindi huo umeifanya Stars iliyokuwa Kundi H kufikisha pointing 10 na kushika nafasi ya pili nyuma ya vinara DR Congo wenye pointi 12 wakati Guinea wanabaki na pointi tisa na Ethiopia wamemaliza wakiwa mkiani na pointi yao moja.
Guinea ni dhahiri wameumizwa mno na matokeo hayo kwani walihitaji sare ya aina yoyote ili kufuzu lakini walijikuta pagumu kwa kipindi kirefu cha mchezo kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya wachezaji wa Stats.
Stars walicheza kwa kujiamini wakikaba na kulishambulia mara kwa mara lango la Guinea ingawa timu hiyo ilikuwa na tatizo katika umaliziaji.
Msuva na Clement Mzize mara kadhaa walilisakama lango la Guinea lakini walikosa umakini katika umaliziaji na kuinyima Stars mabao kabla ya Msuva kurekebisha makosa yake na kuipa Stats ushindi.
Baada ya filimbi ya kumaliza mchezo kupulizwa na mashabiki waliofurika uwanjani kulipuka kwa shangwe, baadhi ya wachezaji wa Guinea walionekana wakimzonga mwamuzi wa mchezo huo katika namna iliyoonesha kutofurahia baadhi ya maamuzi yake.
Stars baada ya ushindi sasa inasubiri kujua itapangwa na timu gani katika Kundi lake kwa ajili ya fainali za Afcon 2025 zitakazofanyika mapema mwakani nchini Morocco.