Manchester, England
Kocha Erik ten Hag aliyetimuliwa katika kikosi cha Man United, ameibuka kwa mara ya kwanza tangu kutimuliwa kwake na kuwashukuru mashabiki kwa namna walivyomuunga mkono.
Ten Hag alitimuliwa Jumatatu iliyopita wakati timu hiyo ikishika nafasi ya 14 kwenye Ligi Kuu England (EPL) ikiwa na rekodi isiyovutia ya kupoteza mechi nne kati ya tisa za mwanzo za ligi hiyo msimu huu wa 2024-25.
Nafasi ya Ten Hag imechukuliwa na kocha kutoka Ureno, Rúben Amorim ambaye hapo kabla alikuwa akiinoa Sporting Lisbon na anatarajia kuanza rasmi kazi hiyo mpya Novemba 11 mwaka huu.
“Nianze kwa kuwashukuru, asanteni kwa wakati wote kuwa karibu na klabu, iwe kwa mechi ya nyumbani au ugenini au mechi ngumu kwenye dimba la Old Trafford, hamkuwahi kuyumba katika kutuunga mkono,” alisema Ten Hag.
Kocha huyo pia aliwashukuru maofisa wa klabu hiyo katika kila idara mbalimbali kwa namna ambavyo walikuwa naye pamoja katika wakati mzuri na hata alipokuwa katika kipindi kigumu.
“Tumeshinda mataji mawili, mafanikio ambayo yataendelea kunifariji katika maisha yangu yote, ni kweli kwamba ndoto zangu zilikuwa ni kuipa klabu hii mataji mengi, bahati mbaya ndoto hiyo haikutimia,” alisema Ten Hag.
Man United ilitangaza rasmi jana Ijumaa uamuzi wa kumkabidhi Amorim majukumu ya Ten Hag ambapo kocha huyo mpya amesaini mkataba utakaofikia ukomo Juni 2027 kukiwa na kipengele kinachotoa nafasi ya kuongeza mwaka mmoja zaidi.