Na mwandishi wetu
Simba imenyakua pointi tatu muhimu ikineemeka na bao pekee la jioni dhidi ya Mashujaa katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa leo Ijumaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Bao hilo pekee lilipatikana dakika ya sita katika dakika za nyongeza baada ya dakika 90 za kawaida kumalizika mfungaji akiwa Lionel Ateba kwa kichwa kufuatia kona iliyochongwa na Awesu Awesu.
Muda mfupi baada ya kuingia bao hilo mwamuzi alipuliza filimbi ya kumaliza mchezo na hapo hapo akajikuta akizongwa na wachezaji wa Mashujaa waliokuwa wakimlalamikia kwa kuchelewa kumaliza mchezo.
Simba sasa imechupa hadi nafasi ya pili ikiwa imefikisha jumla ya pointi 22 ikiwa imefungana pointi na Singida BS lakini zikidiana wastani wa mabao wakati Yanga wakiwa kileleni na pointi zao 24.
Katika mechi yao ya leo, Simba ndio waliokuwa wa kwanza kulisakama lango la Mashujaa katika dakika ya kwanza tu ya mchezo huo baada ya Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ kupanda na mpira mbele.
Zimbwe Jr mara baada ya kupanda mpira huo alimuunganishia Lionel Ateba ambaye hata hivyo shuti lake lilipaa juu ya lango.
Dakika ya 41 Simba walifanya shambulizi jingine safari hii Ateba alimuunganishia pasi Kibu Denis ambaye akiwa katika eneo zuri aliumiki mpira vibaya na kuwahiwa na kipa wa Mashujaa, Eric Johola.
Mashujaa nao mara kadhaa walionekana kulisakama lango la Simba hususan mshambuliaji wake Ismail Mgunda akishirikiana na Seif Abdallah Karie ambao juhudi zao zilikwamishwa na ukuta wa Simba ukiongozwa na kipa Musa Camara.
Ligi hiyo itaendelea Jumamosi kwa mechi kati ya Yanga na Azam kwenye Uwanja wa Azam Complex wakati Singida BS itaumana na Coastal Union kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Soka Bao la jioni laiokoa Simba
Bao la jioni laiokoa Simba
Read also