Na mwandishi wetu
Yanga leo Jumamosi Novemba 2, 2024 imepoteza kwa mara ya kwanza mechi ya Ligi Kuu NBC msimu wa 2024-25 baada ya kulala kwa bao 1-0 mbele ya Azam FC.
Bao hilo pekee katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye dimba la Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, lilifungwa na Gibril Sillah dakika ya 33 akiitumia vizuri pasi ya Adolf Mtasingwa.
Dalili za ushindi kwa Azam zilianza kuonekana dakika ya nane ya mchezo baada ya Paschal Msindo kuitoka safu ya ulinzi ya Yanga na wakati akimkaribia kipa Djigui Diarra aliangushwa chini na Mudathir Yahya.

Tukio hilo liliibua malalamiko kwa wachezaji wa Azam ambao walikuwa wakimlalamikia mwamuzi Ahmed Arajiga kwa imani kwamba alipaswa kuwapa penalti.
Kasi ya Azam iliwaweka Yanga pabaya dakika 10 kabla ya kuingia kwa bao hilo pekee baada ya beki wao wa kati tegemeo, Ibra Bacca kulazimika kumvuta shati Nassor Saaduni aliyemtoka kwa kasi akielekea kukutana na kipa Diarra.
Kwa tukio hilo, Bacca alipewa kadi nyekundu hapo hapo hali ambayo ilizidi kuibua hofu kuhusu hatma ya Yanga kwenye mechi hiyo baada ya kubaki na wachezaji 10 uwanjani.
Yanga nayo mara kadhaa ililichachafya lango la Azam, dakika ya 17, Maxi Nzengeli alimpa Clatous Chama pasi ndefu ambayo aliituliza vizuri na mpira kumsogezea Stephane Aziz Ki ambaye hata hivyo shuti lake halikuwa na madhara.
Dakika ya 88, Yanga ilifanya shambulizi jingine kali kwa mpira ulioanzia kwa Clement Mzize ambaye baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Azam akapiga krosi iliyomkuta Nickson Kibabage ambaye hata hivyo shuti alilopiga lilitoka nje.
Azam baada ya kuwa mbele walianza ujanja wa kuchelewesha muda hali ambayo ilimlazimu mwamuzi wa mchezo huo kumpa kadi ya njano kipa wa timu hiyo, Mohamed Mustapha.
Katika kusaka bao la kusawazisha, kocha wa Yanga Miguel Gamondi alimtoa Chama akaingia Duke Abuya na baadaye akamuingiza Kibabage na kumtoa Shedrack Boka na Prince Dube akatoka nafasi yake akaingia Clement Mzize.
Kocha huyo aliendelea kufanya mabadiliko kwa kumtoa Aziz Ki na nafasi yake kuingia Pacome Zouzoua na Mudathir nafasi yake akaingia Kennedy Musonda mabadiliko ambayo hayakubadili matokeo ya mchezo.
Kwa upande wa Azam walitoka Sillah na Msindo na kuingia Frank Tiesse na Sidibe na baadaye wakatoka Fei Toto na Yeison Fuentes na kuingia Ever Mezer na Yanick Bangala.
Yanga pamoja na kipigo hicho bado inaongoza ligi ikiwa na pointi 24 sawa na Singida BS ambayo nayo leo hii inaumana na Coastal Union japo matokeo ya mechi hiyo yanaweza kuitoa Yanga kileleni.