Manchester, England
Hatimaye klabu ya Manchester United, leo Jumatatu imetangaza kumfuta kazi kocha Erik ten Hag kutokana na mwenendo usiovutia wa timu hiyo tangu kuanza kwa msimu huu wa 2024-25.
Baada ya uamuzi huo, nafasi ya Ten Hag kwa sasa itakaimiwa na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Ruud van Nistelrooy ambaye alikuwa msaidizi wake.
Kutokana na mwenendo mbaya wa Man Utd, habari ya Ten Hag kutimuliwa ilipamba moto siku za karibuni na kutimia kwake ni kama kukamilika kwa tukio ambalo lilikuwa likisubiri siku.
Ten Hag alikuwa uwanjani mara ya mwisho jana Jumapili katika mechi na West Ham, mechi ambayo Man Utd ililala kwa mabao 2-1 na kwa sasa timu hiyo inashika nafasi ya 14 kwenye Ligi Kuu England ikiwa imecheza mechi tisa na kushinda tatu tu.
Taarifa ya klabu hiyo ilieleza kwamba Van Nistelrooy atasimamia masuala ya timu hiyo wakati mchakato wa kumpata kocha mpya wa kudumu ukiendelea huku tayari majina kadhaa yakianza kutajwa likiwamo la aliyekuwa kocha wa Barcelona, Xavi Hernandez.
Uamuzi wa kumtimua Ten Hag ulifikiwa leo asubuhi baada ya kikao cha ana kwa ana kati ya kocha huyo na ofisa mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Omar Berrada pamoja na Dan Ashworth ambaye ni mkurugenzi wa michezo na kocha huyo alielezwa wazi wazi juu ya uamuzi huo.
Baada ya uamuzi huo kufikiwa mchezaji wa kwanza kumtakia kila la heri Ten Hag katika mambo yake ya baadaye ni nahodha wa timu hiyo, Bruno Fernandes ambaye pia alimshukuru kwa kila kitu ikiwamo kwa muda wote ambao wamekuwa pamoja.
Kimataifa Man Utd yamtimua Ten Hag
Man Utd yamtimua Ten Hag
Read also