Na mwandishi wetu
Vigogo vya soka Tanzania, timu za Simba na Yanga zimefanya vizuri katika mechi zake za Ligi Kuu NBC Jumanne hii, Simba ikiichapa Prisons bao 1-0 na Yanga ikiilaza JKT Tanzania kwa mabao 2-0.
Simba ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya ilifaidika na bao hilo pekee mfungaji akiwa ni beki Che Malone Fondoh katika dakika ya tano ya mchezo huo.
Ushindi wa Simba umekuja ikiwa ni siku takriban tatu zimepita tangu icheze na mahasimu wao Yanga na kulala kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.
Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa ligi kuu waliendeleza dhamira yao ya kulitetea taji hilo wakiwa kwenye dimba la Azam Complex kwa ushindi wa mabao ya Pacome Zouzoua dakika ya 23 na Clatous Chama dakika ya 44.
Kwa uushindi huo Yanga sasa imefikisha pointi 18 katika mechi sita ikiwa haijapoteza hata mechi moja na inashika nafasi ya pili nyuma ya Singida BS wanaoshika usukani wakiwa na pointi 19 baada ya kucheza mechi saba.
Kwa upande wa Simba ushindi huo umeifanya timu hiyo kufikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi saba ikiwa imepoteza mechi moja dhidi ya Yanga na kutoka sare mechi moja dhidi ya Coastal Union na inashika nafasi ya tatu.
Soka Simba, Yanga zatamba ligi kuu
Simba, Yanga zatamba ligi kuu
Read also