Na mwandishi wetu
Yanga imepangwa kundi moja na TP Mazembe ya DR Congo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Simba ikipangwa kundi moja na CS Sfaxien ya Tunisia katika Kombe la Shirkisho Afrika.
Makundi hayo yametokana na droo ya michuano hiyo iliyofanyika Jumatatu hii mjini Cairo, Misri yalipo makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Katika droo hiyo mbali na TP Mazembe, Yanga ambayo ipo Kundi A wapinzani wake wengine ni timu za AL Hilal ya Sudan na MC Alger ya Algeria.
Kwa upande wa Simba mbali na CS Sfaxien, timu hiyo iliyo Kundi A pia imepangwa pamoja na timu za FC Bravos Du Maquis ya Angola na CS Constantine ya Algeria.
Meneja Habari wa Simba, Ahmed Ally akizungumzia timu walizopangwa nazo alisema Simba imepangwa na wapinzani wapya ambao hawajawahi kukutana nao hapo kabla wakiwa katika ubora wao..
Akizungumzia malengo yao katika kundi hilo, Ally alisema kwamba wanachotaka ni kumaliza hatua ya makundi wakiwa na alama 16 na kusonga mbele hadi hatua ya robo fainali.
Alifafanua kwamba Simba matarajio yao hayaiishi kwa kwenda robo fainali tu bali kufikia hatua hiyo wakiwa na alama nyingi kwa kuvuka alama 13 walizopata siku za nyuma na kufikisha 16.
Naye Meneja Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema timu yao imepangwa na timu ambazo inazijua lakini tangu awali walishasema wako tayari kucheza na mpinzani yeyote na wakishirikiana kwa pamoja wanaweza kufanya vizuri.
Alisema kwamba wamepata wapinzani ambao anaamini mechi zao hazitakuwa nyepesi ila ni wapinzani ambao wana uwezo wa kushindana nao na kupata matokeo mazuri na hakuna linaloshindikana.