Na mwandishi wetu
Timu ya wanawake ya JKT Queens leo Jumamosi imeibuka kinara wa michuano ya Ngao ya Jamii kwa kuilaza Yanga Princess bao 1-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge, Dar es Salaam.
Bao pekee lililoipa ushindi JKT lilipatikana katika dakika ya 88 ya mchezo huo lilitokana na mpira wa adhabu iliyopigwa nje kidogo ya eneo la 18 na Donisia Minja.
Donisia aliupiga kiufundi mpira uliowavuka wachezaji wa Yanga Princess waliojipanga kuzuia na kumshinda mlinda mlango, Rita Akareko ambaye licha ya juhudi za kuufuata lakini mpira ulijaa wavuni pembeni kupitia upande wake wa kulia.
Katika mechi ya awali ya kusaka mshindi wa tatu iliyopigwa kwenye uwanja huo huo, Simba Queens waliibuka kinara kwa kuichapa Ceassia Queens mabao 4-0.
Mabao ya washindi yalifungwa na Asha Jafar aliyefunga mawili, Precious Christopher na Satra Shamte ambaye alijifunga.
Michuano ya Ngao ya Jamii ndiyo inayofungua pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (TWPL) ambayo kwa msimu wa 2024-25 itaanza kutimua vumbi Oktoba 9 mwaka huu.
Soka JKT Queens yabeba Ngao ya Jamii
JKT Queens yabeba Ngao ya Jamii
Read also