Na mwandishi wetu
Yanga imeendeleza ubabe katika Ligi Kuu NBC baada ya kuichapa Pamba Jiji mabao 4-0 katika mechi iliyopigwa Alhamisi hii jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kwa mara nyingine nyota ya beki wa timu hiyo, Ibrahim Hamas ‘Bacca’ imeendelea kung’ara baada ya kuandika bao la kwanza katika dakika ya tano ya mchezo huo.
Bacca pia ndiye aliyefunga bao pekee la ushindi la timu hiyo katika mechi nyingine ya ligi hiyo dhidi ya Ken Gold, mechi ambayo Yanga ilitoka na ushindi wa bao 1-0.
Stephane Aziz Ki aliihakikishia Yanga kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao mawili baada ya kuandika bao la la pili katika dakika ya 45.
Mambo yaliendelea kuwaharibikia Pamba ambao walijikuta wakibugizwa bao la tatu zikiwa zimepita takriban dakika 10 baada ya timu kutoka mapumziko mfungaji akiwa ni Maxi Nzengeli.
Zikiwa zimebakia dakika tano mpira kumalizika, Kennedy Musonda alikamilisha karamu ya mabao ya Yanga baada ya kufunga bao la nne na kuihakikishia Yanga pointi tatu muhimu.
Mambo yaliwaharibikia zaidi Pamba ambao walilazimika kucheza pungufu kwa kipindi chote cha pili baada ya mchezaji wake Saleh Abdullah kupewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Shedrack Boka wa Yanga.
Kwa ushindi huo Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo sasa wamefikisha pointi 12 katika mechi nne wakiwa hawajapoteza hata mechi moja.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Azam FC ikiwa ugenini ilitoka na ushindi wa bao 1-0 mbele ya Namungo wakati KMC nayo ikiwa nyumbani iliichapa Kagera Sugar bao 1-0.
Soka Yanga yaitandika Pamba 4-0
Yanga yaitandika Pamba 4-0
Read also