Porto, Ureno
Majanga yanazidi kumuandama kiungo na nahodha wa Man United, Bruno Fernandes ambaye jana Alhamisi alipewa kadi nyekundu katika mechi ya Europa Ligi dhidi ya FC Porto iliyoisha kwa sare ya mabao 3-3.
Fernandes alipewa kadi nyekundu baada ya kupewa mbili za njano na hii inakuwa kadi ya pili nyekundu baada ya ile aliyopewa Jumapili katika mechi na Tottenham Hotspur ambayo Man United ililala kwa mabao 3-0.
Kadi aliyopewa katika mechi dhidi ya Spurs hata hivyo ilimfanya asifungiwe mechi tatu baada ya Man United kuikatia rufaa lakini tukio la kupewa kadi kama hiyo katika mechi mbili mfululizo limeshtua.
Katika tukio la mechi dhidi ya Porto, Fernandes alipewa kadi hiyo dakika ya 81 na kuifanya Man United ibaki na wachezaji 10 uwanjani wakati huo huo timu hiyo ilikuwa nyuma kwa mabao 3-2.
Man United hata hivyo iliokelewa na bao la kusawazisha lililofungwa kwa kichwa na beki Harry Maguire katika dakika moja ya nyongeza.
Matokeo yoyote mabaya katika mechi hiyo na Porto huenda yangezidi kumuweka katika wakati mgumu kocha wa timu hiyo Erik ten Hag ambaye ameuanza msimu vibaya.
“Tuliuanza mchezo vizuri na kuutawala, tukafunga mabao mawili mazuri lakini hatimaye tukaanza kupoteza umiliki wa mchezo, mwanzo ulikuwa mzuri katikati ya mchezo tulivurunda lakini mwisho ukawa mzuri,” alisema Ten Hag.
Man United ilikuwa ya kwanza kupata mabao ya Marcus Rashford na Rasmus Højlund na kuongoza kwa 2-0 kabla ya Porto kusawazisha kupitia Pepe na Samu Omorodion. Kipindi cha pili Omorodion tena aliiongezea Porto bao la tatu.