Na mwandishi wetu
Timu ya soka ya wanawake ya Yanga Princess imeibuka kidedea katika mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii kwa kuwalaza mahasimu wao wa Simba Queens kwa penalti 4-3.
Kwa ushindi huo, Yanga Princess wanasubiri kuumana na JKT Queens ambao katika mechi ya awali waliibugiza Ceasiaa Queens mabao 7-0. Mechi zote hizo zilipigwa kwenye Uwanja wa KMC, Kinondoni, Dar es Salaam.
Katika mechi ya mahasimu, Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika za awali lililofungwa na Agnes Palangyo bao ambalo lilidumu kwa dakika zote 45 za kwanza.
Simba Queens walipambana na juhudi zao kuzaa matunda zikiwa zimebakia dakika mbili kabla ya mchezo kumalizika kwa kupata bao lililofungwa na Jentrix Shikangwa na hatimaye timu hizo kupigiana penalti.
Simba baada ya kupoteza mchezo huo sasa wataumana na Ceasiaa Queens katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu, ambayo kama ilivyo mechi ya fainali, zote zitapigwa Jumamosi ya Oktoba 5 mwaka huu.
Michuano ya Ngao ya Jamii kwa wanawake inaashiria ufunguzi wa Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake (TWPL) ambayo inashirikisha timu 10 na kwa msimu huu wa 2024-25 itaanza rasmi kutimua vumbi Oktoba 9.
Soka Simba Queens hoi kwa Yanga Princess
Simba Queens hoi kwa Yanga Princess
Read also