Na mwandishi wetu
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ina mechi mbili muhimu dhidi ya timu ya taifa ya DR Congo ili kuthibitisha uwezo wake katika mbio za kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Africa (Afcon) 2025.
Stars iliyo kundi H itaanzia ugenini Oktoba 10 na kurudiana na timu hiyo Oktoba 15 jijini Dar es Salaam, mechi ambazo Stars ikishinda zote itajikusanyia pointi sita na hivyo kufikisha jumla ya pointi 10.
Awali timu hiyo ilianza hovyo mechi ya kwanza na Ethiopia kwa sare ya bila kufungana, tena ikiwa kwenye uwanja wa nyumbani kabla ya kupata ushindi katika mechi ya pili ugenini dhidi ya Guinea.
Kwa hiyo ushindi dhidi ya DR Congo kwanza utakuwa umefunika makosa ya awali ya sare ya bila kufungana na Ethiopia lakini pia utadhihirisha uwezo na dhamira ya timu hiyo kufuzu Afcon 2025.
Stars tayari imeshaonesha uwezo ugenini katika mechi na Guinea, ushindi ilioupata wa mabao 2-1 umeonesha kwamba timu hiyo iko vizuri ina uwezo na kilichotokea dhidi ya Ethiopia ni makosa ya kawaida.
Matokeo yoyote mabaya baada ya sare na Ethiopia na ushindi dhidi ya Guinea yatafifisha matumaini ya timu hiyo kuelekea Afcon 2025.
Kwa hiyo mechi mbili za Stars dhidi ya DR Congo zimebeba mwelekeo wa timu hiyo na ndizo zinazoweza kuthibitisha kila kitu kama Stars hii inaelekea kufuzu Afcon 2025 au nafasi yake ni ndogo au haipo.
Matokeo yoyote mabaya dhidi ya DR Congo yanaweza kuwa mwanzo wa kuitoa timu hiyo kwenye mstari au kuiweka katika wakati mgumu na kujikuta ikilazimika kuangalia matokeo ya timu nyingine ili kujua kama inafuzu Afcon 2025 au la.
Stars ikiwa tayari imecheza mechi mbili inatakiwa ihakikishe inashika usukani katika kundi lake yaani Kundi H na hilo litawezekana au kuwa rahisi iwapo itapata matokeo mazuri katika mechi dhidi ya DR Congo.
Baada ya mechi mbili za Stars, DR Congo inaonekana kuwa timu ngumu kwenye kundi la Stars na hivyo ili kujiwekea mazingira mazuri ya kufuzu, mechi na timu hiyo inabaki kuwa kikwazo muhimu cha kukivuka.
Guinea na Ethiopia japo si timu nyepesi lakini tayari Stars imeonesha ina uwezo mkubwa wa kuzifunga katika mechi za marudiano na hatimaye kumaliza mechi zake zote ikiwa na jumla ya pointi 16.
Bila kujali matokeo ya timu nyingine, pointi 16 zinatosha kuifanya Stars iwe katika nafasi nzuri ya kujikatia tiketi ya kushiriki Afcon 2025.
Dr Congo ndio wanaoongoza kundi hilo wakiwa na pointi sita wakifuatiwa na Stars wenye pointi nne na wa tatu ni Ethiopia wenye pointi moja na Guinea wanashika mkia wakiwa hawana pointi hata moja.
Kimataifa Mechi ya DR Congo, kikwazo muhimu Stars kukivuka
Mechi ya DR Congo, kikwazo muhimu Stars kukivuka
Read also