Na mwandishi wetu
Simba imetoka kifua mbele kwenye dimba la New Amaan, Zanzibar baada ya kuilaza Azam FC mabao 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyochezwa leo Alhamisi usiku.
Bao la kwanza la Simba lilipatikana dakika ya 15 mfungaji akiwa Lionel Ateba aliyeinasa pasi ndefu ya Jean Ahoua na kuonesha utulivu kabla ya kuihadaa safu ya ulinzi na kufumua shuti lililojaa wavuni.
Simba iliendelea kulisakama lango la Azam na katika dakika ya 28, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ aliambaa na mpira kutokea upande wa kushoto na kuupiga moja kwa moja kwenye lango la Azam lakini kipa Mohamed Mustapha alikuwa makini.
Dakika moja baadaye Azam walijibu mapigo ambapo Feisal Salum ‘Fei Toto alionesha uwezo wake wa kufumua mashuti ya mbali na safari hii alimpima kipa wa Simba, Musa Camara kwa shuti kali la juu.
Shuti hilo lililowaamsha vitini mashabiki wa Azam liligonga mwamba wa goli na kutoka nje huku kipa Camara naye akionesha umakini kwa kuufuata mpira ingawa ulimpita na kugonga mwamba.
Dakika mbili baada ya timu kutoka mapumziko, Simba waliandika bao la pili lililofungwa na Donald Ngoma, bao ambalo lilitokana na mpira wa adhabu uliopigwa na Ahoua kabla ya kumkuta mfungaji.
Katika mechi hiyo makocha wa timu zote mbili walifanya mabadiliko kwa Simba ikiwatoa Ahoua, Ateba, Kibu na Debora Fernades na nafasi zao kuingia Awesu, Mukwala, Kelvin Kijili na Augustine Okejepha.
Kwa Azam walitoka Jibri Sillah, Iddi Nado na Nassor Saadun na nafasi zao kuingia Cheikh Sidibe, Cheikna Diakite na Alfonso Blanco.
Soka Simba yaitandika Azam 2-0
Simba yaitandika Azam 2-0
Read also