Madrid, Hispania
Liverpool imeanza kupiga hesabu za kumsajili mshambuliaji wa Real Madrid, Rodrygo ili achukue nafasi ya Mohamed Salah baada ya kuwapo habari kwamba Salah anajipanga kuihama timu hiyo.
Hivi karibuni, Salah, 32, mshambuliaji tegemeo wa Liverpool na timu ya taifa ya Misri, japo hakuwa wazi lakini alisema huu unaweza kuwa msimu wake wa mwisho kuvaa jezi ya Liverpool.
Kauli hiyo inaonesha kwamba huenda Liverpool ikamkosa mshambuliaji huyo ambaye kwa muda mrefu amekuwa akiwindwa na klabu kadhaa za Saudi Arabia na ndio maana Liverpool imeanza mapema hesabu za mtu wa kuziba nafasi hiyo.
Katika harakati hizo, chanzo kimoja cha habari kimeripoti kuwa jina la Rodrygo, ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya Brazil ndilo linalotajwa zaidi na kuonekana anaweza kuwa mtu sahihi wa kuchukua nafasi hiyo.
Kwa upande wa Rodrygo kinachoonekana ni kwamba huenda akawa tayari kwa changamoto mpya hasa kutokana na ushindani wa namba ambao unatajwa katika kikosi cha kwanza cha Real Madrid.
Tangu Real Madrid imsajili Kylian Mbappe kumekuwa na hofu kuhusu nafasi ya Rodrygo ingawa kocha Carlo Ancelotti amekuwa akiwapa nafasi washambuliaji watatu kwenye kikosi cha kwanza.
Msimu uliopita, Real Madrid ilibeba mataji ya La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo kwa La Liga Rodrygo alifunga mabao 10 katika mechi 34 na kwa Ligi ya Mabingwa alifunga mabao matano.
Rodrygo, 23, pamoja na kufunga mabao hayo, jina lake halimo katika wachezaji wanaowania tuzo ya Ballon d’Or jambo ambalo alisema limemsikitisha kwa kuwa anaamini alipaswa kuwamo.
Wachezaji wa Real Madrid waliomo katika orodha ya wanaowania tuzo hiyo ni VinÃcius Júnior, Jude Bellingham, Federico Valverde, Toni Kroos, Antonio Rüdiger, Dani Carvajal na Mbappe.