Na mwandishi wetu
Simba imefuzu hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuichapa Ahly Tripoli ya Libya mabao 3-1 katika mechi iliyopigwa Jumapili hii jioni Septemba 22, 2024 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Ahly walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 17 lililofungwa na mshambuliaji hatari wa timu hiyo, Paciencia Mabululu, bao lililowaduwaza mashabiki wa Simba na kuwafanya wasielewe nini kilichowakuta.
Kibu Dennis aliwatuliza mashabiki hao katika dakika ya 36 baada ya kusawazisha bao hilo akiitumia vizuri pasi ya kichwa ya Che Malone Fondoh, bao ambalo liliwarudisha Simba katika ubora wao.
Wachezaji wa Simba waliendelea kulisakama lango la Ahly ambao ni kama walianza kujichanganya na Simba kuutumia mwanya huo kuandika bao la pili lililofungwa na Lionel Ateba dakika ya 45.
Ahly baada ya kuona mambo yanakwenda ndivyo sivyo walianza kufanya mabadiliko ikiwamo kumuingiza mshambuliaji wao mahiri Ahmed Arawa aliyechukua nafasi ya Ghaelin Shelel.
Simba nao walijiimarisha kwa mabadiliko kadhaa kwa kuwatoa Yusuf Kagoma, Kibu, Joshua Mutale na Jean Ahoua na nafasi zao kuingia Donald Ngoma, Okejepha Augustine, Edwin Balua na Kelvin Kijili.
Mabadiliko hayo yalikuwa na maana kubwa kwa Simba ambao waliandika bao la tatu lililofungwa na Balua katika dakika ya 90 baada ya kuambaa na mpira na kufumua shuti la chinichini lililomshinda kipa.
Dakika ya 61 Simba ilipata bao lililofungwa na Ateba baada ya Ahoua kumchambua kipa wa Ahly, Ayman Abdullah na kumpasia Ateba lakini bao lilikataliwa kwa madai kuwa mpira uliomfikia Ahoua kutoka kwa Deborah Fernandes ulizaa tukio la kuotea.
Ahly walilitikisa lango la Simba baada ya kufungwa bao la pili wakitaka kuwasazisha, Mabululu aliunasa mpira uliotokana na kona na kuupiga kwa juu lakini kipa wa Simba, Mussa Camara aliyekuwa tayari amehama upande, alionesha umahiri wake kwa kuuwahi mpira huo na kuokoa huku akiwalaumu mabeki wake kwa uzembe.
Baada ya mechi hiyo Ahly walianza kumzonga mwamuzi wakimlaumu tukio ambalo lilimfanya mwamuzi huyo atoe kadi nyekundu ambayo alimpa mshambuliaji wa timu hiyo, Mabululu.
Kwa matokeo hayo, Simba sasa inasubiri kucheza hatua ya makundi ikiwa imefuzu kwa jumla ya mabao 3-1 baada ya sare ya bila kufungana katika mechi ya kwanza iliyochezwa juma lililopita mjini Tripoli, Libya. Wakati huo huo Simba pia inapata zawadi ya Sh milioni 15 zinazotokana na ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya Sh milioni tano kwa kila bao linalofungwa kwenye mechi ya ushindi ya michuano hiyo.
Kimataifa Simba yairarua Ahly Tripoli 3-1
Simba yairarua Ahly Tripoli 3-1
Read also