Porto, Ureno
Winga wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo amemtaja mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappé kuwa ni mchezaji ambaye ana nafasi ya kubeba tuzo ya Ballon d’Or.
Akizungumza kupitia chaneli ya You Tube, Ronaldo pia alisema kwamba Mbappe atapata mafaniko katika klabu ya Real Madrid ambayo alisema kwake itabaki kuwa ndiyo klabu bora.
Ronaldo alisema kwamba anafikiri Mbappe atafanya vizuri na kuutaja muundo wa klabu hiyo kuwa ni mzuri na upo sawa.
“Wana kocha bora, Carlo Ancelotti na raisi Florentino (Perez) ambaye yupo pale kwa miaka mingi, nafikiri haitokuwa tatizo kubwa kwa sababu Mbappe ana kipaji, atakuwa mshindi ajaye wa Ballon d’Or, yeye (Erling) Haaland, (Jude) Bellingham, Lamine (Yamal),” alisema Ronaldo.
Akiizungumzia zaidi Real Madrid, Ronaldo alisema ni aina ya timu ambayo haina presha, ingawa kuna wanaosema ina bahati kwenye Ligi ya Mabingwa, Ronaldo anakataa hilo badala yake anasema ni timu inayojiandaa kwa matukio ya aina hiyo na hata uwanja wao (Bernabéu) ipo kivingine kabisa.
“Kwa sasa huwezi kusema kama Real Madrid itakuwa timu bora au la, hatujui, Mbappe yupo pale kwa sasa, nafikiri itaendelea kuwa timu imara ingawa sijui kama itakuwa hivyo kuliko msimu uliopita, Mungu tu ndiye anayejua,” alisema Ronaldo.
Ancelotti aliwahi kumzungumzia Mbappe akisema wanaendelea kujizoeza maisha ya kuwa na nyota huyo ambaye ameonesha kila dalili za kuanza kuwa bora akiwa na mabao mawili dhidi ya Real Betis kabla ya kwenda kuitumikia timu ya taifa.
Real Madrid imeshinda mechi zake mbili na kutoka sare mbili katika mechi nne za msimu huu ikiwa nafasi ya pili kwenye La Liga nyuma ya mahasimu wao, Barcelona kwa tofauti ya pointi nne.