Madrid, Hispania
Mshambuliaji wa Real Madrid, Rodrygo ameelezea namna alivyovurugwa na kukatishwa tamaa kwa kitendo cha jina lake kutokuwemo kwenye orodha ya wachezaji 30 wanaowania tuzo ya Ballon d’Or.
Rodrygo ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil, msimu uliopita alitoa mchango mkubwa kwa Real Madrid hadi kubeba mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu Hispania au La Liga.
Wachezaji wenzake wa Real Madrid, Vinícius Júnior, Jude Bellingham, Federico Valverde, Toni Kroos, Antonio Rüdiger na Dani Carvajal wamo katika orodha hiyo pamoja na mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Kylian Mbappe lakini Rodrygo hayumo.
“Nimekatishwa tamaa, nadhani ninafaa kuwamo, sitaki kuwashushia hadhi wachezaji walio katika orodha hyo lakini nafikiri nafasi yangu imo kwenye orodha ya wachezaji 30, imenishangaza ingawa hakuna ninachowza kufanya, mimi sina maamuzi katika mambo haya,” alisema Rodrygo.
Rodrygo anajivunia kuifungia Real Madrid mabao 10 katika mechi 34 za La Liga msimu uliopita lakini pia alifunga mabao matano kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Nafasi ya Rodrygo kwenye kikosi cha kwanza cha Real Madrid imekumbana na changamoto tangu kusajiliwa kwa Mbappe ingawa kocha wa timu hiyo, Carlo Ancelotti ameendelea kumpa nafasi akiwa miongoni mwa washambuliaji watatu wa kikosi cha kwanza.
Kimataifa Orodha Ballon d’Or yamvuruga Rodrygo
Orodha Ballon d’Or yamvuruga Rodrygo
Read also