Na mwandishi wetu
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo Jumatano imezianza mbio za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 kwa sare ya bila kufungana na timu ya taifa ya Ethiopia.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, Ethiopia walitawala vyema kipindi cha kwanza kwa kuumiliki mpira wakiwa wametulia na kukicheza pasi za uhakika.
Kwa muda mrefu wa kipindi hicho Stars walikuwa na kazi ya kuusaka mpira na hata walipoupata hawakuweza kucheza pasi nyingi badala yake Ethiopia waliwatibulia na kuendelea kuutawala mchezo huo.
Mambo yalianza kubadilika kwa upande wa Stars katika kipindi cha pili baada ya kocha Ahmed Suleiman ‘Morocco’ kumtoa Nickson Kibabage na nafasi yake kuingia Paschal Msindo.
Msindo aliinasa pasi ya chini aliyopenyezewa na Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’ na kupiga krosi ambayo Fei Toto aliunganisha kwa kichwa lakini kipa wa Ethiopia aliokoa na kuwa kona ambayo haikuwa na madhara.
Dakika ya 58 Morocco aliendelea kufanya mabadiliko kwa kuwatoa Himid Mao na Balua na nafasi zao kuingia Mudathir Yahya na Waziri Junior ambao waliiongezea uhai Stars na kuzidi kulichachafya lango la Ethiopia.
Stars kwa mara nyingine ilifanya mashambulizi dakika za 72 na 73 yaliyozaa mashuti yaliyopigwa na Mudathir na Fei Toto na baadaye kuzaa mpira wa adhabu uliopigwa na Novatus Miroshi lakini kipa wa Ethiopia Seid Habtamu Aregawi alikuwa makini.
Dakika ya 78, Mudathir alimpenyezea pasi Waziri Junior ambaye aliukimbilia mpira lakini kipa wa Ethiopia naye akatoka langoni kwa haraka na kuuwahi mpira huo.
Zikiwa zimebaki dakika mbili kabla ya kutimia dakika 90, Stars walifanya shambulizi lililowainua mashabiki vitini baada ya Clement Mzize kumpasia Mudathir ambaye shuti lake la chini lilitoka sentimita chache nje ya lango la Ethiopia.
Stars itajitupa tena uwanjani Jumanne Septemba 10 kwa kucheza mechi yake ya pili ikiwa ugenini dhidi ya Guinea.
Kimataifa Stars, Ethiopia hakuna mbabe
Stars, Ethiopia hakuna mbabe
Read also