Liverpool, England
Mshambuliaji wa timu ya Liverpool, Mohamed Salah amesema kwamba huenda huu ukawa msimu wake wa mwisho kuichezea timu hiyo.
Salah ambaye jana Jumapili aliiwakilisha Liverpool katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Man United kwenye Ligi Kuu England (EPL), mkataba wake na timu hiyo unafikia ukomo mwishoni mwa msimu huu wa 2024-25.
Katika mechi hiyo, Salah, 32, ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya taifa ya Misri, alifunga bao moja na kutoa asisti mbili.
“Nimekuwa na kipindi kizuri cha mapumziko ya kiangazi, nimekuwa na muda mrefu wa kukaa peke yangu na kufikiria mazuri, kama unavyofahamu huu ni mwaka wangu wa mwisho katika klabu hii,” alisema Salah.
Salah alisema anachotaka ni kuufurahia msimu huu na hadhani kama atakuwa mtu mwenye fikra nyingi badala yake anachoona ni kwamba yuko huru kucheza soka na mambo yajayo yatajulikana.
“Hakuna mtu yeyote aliyezungumza nami kuhusu mkataba wangu, kwa hiyo kilicho sahihi ni kuwa nitacheza katika msimu wangu wa mwisho na baada ya msimu tutaona itakavyokuwa, si juu yangu,” alisema Salah.
Septemba mwaka jana Liverpool ilikataa ofa ya Pauni 150 milioni kutoka klabu ya Al Ittihad ya Saudi Arabia na ingawa zipo habari za klabu hiyo kuanza upya mpango wa kumtaka Salah lakini jambo hilo bado halijawa rasmi.
Kwa upande wake kocha wa Liverpool, Arne Slot alisema kwamba hatojadili suala la mchezaji huyo kuhusu mkataba wake badala yake anachofahamu ni kwamba Salah ni mchezaji wao na jambo hilo linampa furaha.
Wachezaji wengine wa Liverpool ambao mikataba yao inafikia ukomo mwishoni mwa msimu huu ni pamoja n nahodha Virgil van Dijk na Trent Alexander-Arnold.
Kimataifa Salah atangaza kuondoka Liverpool
Salah atangaza kuondoka Liverpool
Read also