London, England
Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya England, David Beckham ametuma salamu za pole kufuatia kifo cha kocha wa zamani wa timu hiyo, Sven-Goran Eriksson aliyemtaja kuwa ni mtu muungwana na ataendelea kumshukuru.
Eriksson ambaye anatokea nchini Sweden, ni kocha wa kwanza wa kigeni kuifundisha timu ya taifa ya England amefariki dunia Jumatatu hii kwa maradhi ya saratani (kansa) akiwa na miaka 76.
Mwaka 2001, Eriksson alimteua Beckham kuwa nahodha wa timu hiyo ambapo mchezaji huyo amemshukuru kwa namna ambavyo amekuwa mtu mzuri kwake.
“Sven, ahsante kwa namna ambavyo umekuwa mtu mzuri kwa wakati wote, umekuwa mwenye kujali, mtulivu, msikivu na muungwana wa kweli, nitaendelea kukushukuru kwa kunifanya nahodha wako,” alisema Beckham ambaye pia alizichezea timu za Man United na Real Madrid.
Beckham sambamba na ujumbe huo aliouweka kwenye mitandao ya kijamii pia aliambatanisha picha yake alipomtembelea kocha huyo mapema mwaka huu.
Januari mwaka huu Eriksson aliibua mshtuko baada ya kutangaza hadharani kuwa ana maradhi ya saratani na kufafanua zaidi kwamba hana muda mrefu wa kuendelea kuishi duniani.
“Tulicheka, kulia na tulifahamu kwamba tunaagana, nitaendelea kubaki na kumbukumbu za siku hiyo nikiwa nawe na familia yako, ahsante Sven na kauli yako ya mwisho ni kwamba mambo yatakuwa sawa,” alisema Beckham.
Akiwa na timu ya taifa ya England kati ya mwaka 2001 hadi 2006, Eriksson aliiongoza timu hiyo na kuifikisha hatua ya robo fainai ya Kombe la Dunia na fainali za Euro.
Mbali na timu ya taifa ya England, Eriksson pia amewahi kuzinoa klabu 12 tofauti zikiwamo za Leicester City, Man City, Roma Lazio na kwa ujumla ana rekodi ya kushinda mataji 18 tofauti.
Naye mshambuliaji wa zamani wa England, Wayne Rooney ambaye akiwa na miaka 17 aliitwa mara ya kwanza kwenye timu ya England na Eriksson alimtaja kocha huyo kuwa ni mtu wa kipekee na kumtakia mapumziko mema.