Na mwandishi wetu
Yanga leo Jumamosi imeilaza Vital’O ya Burundi mabao 6-0 na kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Azam FC ikitupwa nje ya michuano hiyo kwa kipigo cha mabao 2-0 mbele ya APR ya Rwanda.
Ushindi wa Yanga iliyokuwa kwenye Uwanja wa Azam Complex unaifanya timu hiyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 10-0 baada ya ushindi wa mechi ya kwanza wa mabao 4-0.
Yanga sasa inasubiri kuumana na Commercial Bank of Ethiopia (CBE) ambayo imesonga mbele baada ya kuitoa Sports Club Villa ya Uganda kwa jumla ya mabao 3-2.
Ukurasa wa mabao ya Yanga ulifunguliwa dakika ya 13 kwa bao la mkwaju wa penalti uliojazwa wavuni kiufundi na Pacome Zouzoua.
Penalti hiyo ilitotolewa baada ya mchezaji wa APR, Amedee Ndavyutse kutumia mkono kuokoa shuti la Pacome lililokuwa likielekea langoni mwa APR na kabla ya kutoa penalti hiyo mwamuzi alimpa Amedee kadi nyekundu.
APR wakiwa pungufu uwanjani walipambana na kufanikiwa kumaliza nusu ya kwanza ya mchezo wakiwa nyuma kwa bao hilo pekee kabla balaa halijaanza kuwaangukia kipindi cha pili.
Dakika tatu baada ya kuanza kipindi hicho, Yanga waliandika bao la pili lililofungwa na Clement Mzize wakati bao la tatu lilifungwa na Clatous Chama katika dakika ya 50.
Prince Dube aliandika bao la nne dakika ya 72 kabla Stephane Aziz Ki na Mudathir Yahya hawajakamilisha karamu ya mabao ya Yanga kwa kutupia nyavuni katika dakika za 79 na 86.
Yanga leo ilizidi kuwa moto kipindi cha pili wakati Vital’O ikipata pigo baada ya mchezaji wake mwingine kupewa kadi nyekundu na hivyo kubaki na wachezaji tisa uwanjani.
Vital’O ilijikuta ikiwa na kazi ngumu ya kuokoa, lango lao lilishambuliwa mara kwa mara huku kipa wa Yanga, Djigui Diarra kwa kipindi kirefu akiwa kama hayupo uwanjani kwa namna alivyokosa misukosuko ya mara kwa mara.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alifanya mabadiliko kadhaa yaliyozidi kuipa uhai Yanga katika kipindi cha pili akimtoa Aziz Andambwile na kumuingiza Aziz Ki.
Wachezaji wengine ambao Gamondi aliwatoa ni Clement Mzize, Kennedy Musonda, Pacome na Duke Abuya na nafasi zao kuingia Prince Dube, Mudathir Yahya, Salum Aboubakar na Maxi Nzengeli.
Baada ya kuwatoa Vital’O Yanga pia wana kila sababu ya kufurahia zawadi ya Sh milioni tano kwa kila bao walilofunga maarufu ‘Zawadi ya Mama’ ambayo imetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa timu zinazoshiriki michuano ya klabu Afrika.
Kwa upande mwingine mambo si mazuri kwa Azam ambao katika hali isiyotarajia walishindwa kuulinda ushindi wao wa bao 1-0 walioupata dhidi ya APR katika mechi yao ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Azam wamechapwa mabao 2-0 na APR wakiwa ugenini Rwanda na sasa watarudi nyumbani wakiwa wametolewa kwa jumla ya mabao 2-1.
Kimataifa Yanga yaipiga Vital’O 6-0, Azam hoi
Yanga yaipiga Vital’O 6-0, Azam hoi
Read also