Madrid, Hispania
Mshambuliaji wa Real Madrid, Vinícius Júnior atalazimika kusubiri hadi mwishoni ma msimu huu kabla ya kuamua kama atakwenda kucheza soka Saudi Arabia au ataendelea kukipiga Real Madrid.
Katika wiki chache zilizopita habari za mchezaji huyo kutakiwa kwenye Ligi Kuu Saudi Arabia maafufu Saudi Pro League zimekuwa zikisikika ingawa haijawekwa wazi timu inayomhitaji.
Vinicius ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil kwa sasa ana mkataba na Real Madrid unaofikia ukomo mwaka 2027 na hajasema lolote kuhusu mpango huo licha ya kuwa gumzo kwenye vyanzo kadhaa vya habari.
Inadaiwa wawakilishi kutoka kampuni moja ya Saudi Arabia wamewasiliana na wakala wa mchezaji huyo ambaye pia amekuwa akitajwa kuwa na uwezekano wa kubeba tuzo ya Ballon d’Or,
Wawakilishi hao hata hivyo hawajaweka wazi ofa yao badala yake wameonesha nia yao ya kumtaka mshambuliaji huyo japo upo uwezekano wa Real Madrid kuwa wagumu kuikubali ofa hiyo.
Jambo pekee ambalo wawakilishi hao wameanza kulifanyia kazi ni mshahara mnono wa Vinicius akiwa Saudi Arabia na baada ya hapo wawasilishe ofa rasmi katika klabu ya Real Madrid.
Saudi Arabia ambao wanajiandaa kuwa wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2034, wanaamini kuwa na mchezaji wa hadhi ya Vinicius ni jambo lenye maana kubwa katika kampeni ya kutangaza soka la nchi hiyo.
Vinicius ambaye ana mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya pamoja na matatu ya La Liga akiwa na Real Madrid, habari zaidi zinadai kwamba mpango huo wa kwenda Saudi Arabia ukikamilika huenda akawa mwanamichezo anayelipwa fedha nyingi.
Kimataifa Vinicius kwenda Saudia ni suala la muda
Vinicius kwenda Saudia ni suala la muda
Read also