Madrid, Hispania
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema kitendo cha mshambuliaji wake mpya, Kylian Mbappe kushindwa kuzifumania nyavu katika mechi mbili mfululizo za La Liga hakimsumbui.
Mbappe amejiunga na Real Madrid kwa mkataba wa miaka mitano huu ukiwa msimu wake wa kwanza na ingawa mambo hayajawa mazuri kwenye La Liga, tayari ameifungia timu hiyo bao katika mechi ya Uefa Super Cup dhidi ya Atalanta mapema mwezi huu.
Usajili wa Mbappe Real Madrid ulikuwa gumzo duniani kote lakini bado hajaanza kutema cheche zake na Jumapili katika mechi na Real Valladolid licha ya Real Madrid kushinda kwa 3-0 lakini Mbappe alitupwa benchi dakika ya 86.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Ancelotti alipingana na hoja kwamba Mbappe anashindwa kufunga kwa sababu anacheza nafasi ya mshambuliaji wa kati badala ya pembeni.
“Hapana, sidhani kama kuna hilo tatizo hata kidogo, Mbappe ni mshambuliaji wa kipekee, ana kasi na anakwenda vizuri hata asipokuwa na mpira,” alisema Ancelotti.
Akifafanua zaidi kuhusu Mbappe katika mechi na Valladolid, Ancelotti alisema mshambuliaji huyo alipata nafasi tatu na anaamini katika nafasi hizo ataweza kufunga kama ambavyo amekuwa akifunga mara zote na hadhani kama ili kufunga ni lazima acheze kushoto au kulia.
Katika hatua nyingine, Ancelotti pia alimpongeza Endrick ambaye amesaini timu hiyo msimu huu mara baada ya kufikisha miaka 18.
Alisema kwamba mchezaji huyo ni hazina na akiwa kwenye lango ameonesha uwezo wake wote, anamiliki vizuri mpira na anapiga mashuti vizuri.
Kimataifa Ancelotti hana hofu na Mbappe
Ancelotti hana hofu na Mbappe
Read also