Na mwandishi wetu
Yanga imezianza fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kishindo baada ya kuibugiza Vital’O ya Burundi mabao 4-0, mechi iliyopigwa leo Jumamosi kwenye dimba la Azam Complex, Dar es Salaam.
Prince Dube ndiye aliyekuwa wa kwanza kuwainua vitini mashabiki wa Yanga alipoandika bao la kwanza dakika ya tano tu ya mchezo akiyatumia makosa ya beki wa Vital’O aliyejichanganya wakati akiokoa mpira.
Vital’O licha ya kuonekana kuwa timu dhaifu mbele ya Yanga lakini kuingia kwa bao hilo bado haikuwa tatizo kwao, waliendelea kucheza soka la kutulia wakijihami na kusogelea langoni mwa Yanga mara chache.
Hali hiyo iliwaweka Yanga pagumu na haikushangaza hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Yanga walikuwa mbele kwa bao hilo pekee la Dube.
Kipindi cha pili hata hivyo mambo yalikuwa magumu kwa Vital’O ambao katika dakika ya 70 walipachikwa bao la pili mfungaji akiwa Clatous Chota Chama.
Dakika mbili tu baada ya kuingia bao hilo, Clement Mzize aliwainua tena vitini mashabiki wa timu hiyo alipopachika bao la tatu kabla ya Stephane Aziz Ki hajakamilisha karamu ya mabao dakika ya 89 kwa kuandika bao la nne.
Aziz Ki alifunga bao hilo kwa mkwaju wa penalti ambayo ilitolewa baada ya mchezaji huyo kufanyiwa madhambi wakati akielekea kuonana na kipa wa Vital’O, Hussein Ndiyeshimana.
Matokeo hayo yameiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kusonga mbele na sasa inachohitaji ni sare au ushindi wa aina yoyote katika mechi ya marudiano ambayo pia itapigwa jijini Dar es Salaam hapo Agosti 24.
Ikimalizana na Vital’O Yanga itakuwa na kibarua cha pili katika michuano hiyo kwa msimu huu wa 2024-25 kwa kuumana na mshindi wa mechi kati ya SC Villa ya Uganda na Commercial Bank ya Ethiopia ambazo pia zinaumana hii leo jijini Kampala, Uganda.
Kimataifa Yanga yaibugiza Vital’O 4-0
Yanga yaibugiza Vital’O 4-0
Read also