Manchester, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag ameonesha kuwa na wasiwasi na timu yake kama ipo tayari kwa mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu England (EPL) msimu wa 2024-25 dhidi ya Fulham, leo Ijumaa.
Man United itakuwa nyumbani katika mechi hiyo ya kwanza ambapo wachezaji wake wapya Noussair Mazraoui na Matthijs de Ligt watakuwa kwenye kikosi cha timu hiyo wakiwa ndio kwanza wamewasili Alhamisi na hivyo kumuweka njia panda Ten Hag kuhusu kuwapa nafasi au la.
Sambamba na hilo Ten Hag ana janga la majeruhi kuanzia kwa Luke Shaw, beki mpya Leny Yoro na mshambuliaji Rasmus Hojlund ambao kila mmoja ana matatizo yake ambapo kwa Yoro imebainika atakuwa nje kwa miezi mitatu.
Katika usajili wa wachezaji wapya Man United imemwaga kitita cha Pauni 60 ili kuwanasa Mazraoui na De Ligt kutoka Bayern lakini uhakika wa kuwatumia katika mechi ya leo ni jambo linalomtatiza Ten Hag.
“Timu hii haijawa tayari lakini ligi ndio inaanza, ni dhahiri kuna makocha wengine wengi wenye tatizo kama hili lakini ni lazima tuanze, hatuwezi kujificha katika hilo, hatuwezi kulikimbia, ni lazima tukabiliane nalo,” alisema Ten Hag.
Eneo la beki wa kushoto ni tatizo jingine litakalomuweka njia panda Ten Hag katika kuamua nani wa kumpanga kwa kuwa Shaw hayuko fiti wakati Tyrell Malacia naye ni majeruhi na atakuwa nje kwa miezi miwili akijiuguza hoti.