Na mwandishi wetu
Baada ya mvutano wa siku kadhaa hatimaye klabu za Simba na KMC zimefikia makubaliano kuhusu mchezaji Awesu Awesu ambaye sasa ataitumikia Simba badala ya timu yake ya zamani ya KMC.
Na tayari mchezaji huyo wa nafasi ya kiungo amejiunga na kambi ya Simba au Mnyama kwa ajili ya mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu NBC msimu wa 2024-25 dhidi ya Tabora United utakaopigwa Jumamosi hii.
Awesu ambaye alisajiliwa na Simba, uongozi wa KMC ulipinga usajili huo na kudai kwamba taratibu za usajili zilikiukwa na hivyo kulifikisha suala hilo katika kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ambayo iliipa ushindi KMC.
Baada ya uamuzi wa kamati hiyo, viongozi wa klabu hizo mbili walikutana na kufikia makubaliano na kumfanya Awesu ambaye alinukuliwa akisema kwamba yuko tayari kwenda kuuza samaki kuliko kurudi KMC lakini sasa amepata uhalali wa kuichezea Simba.
Taarifa ya KMC iliyopatikana Alhamisi hii ilikiri kufikiwa kwa makubaliano hayo na kumtakia nahodha huyo wa zamani wa KMC kila la heri baada ya kuitumikia timu hiyo kwa takriban miaka miwili.
Awesu aliamua kuvunja mkataba na KMC na kuilipa timu hiyo kiasi cha Sh 50 milioni na Simba ilimtambulisha kama mchezaji huyo kabla ya KMC kuwasilisha malalamiko TFF na hatimaye Simba kujikuta katika mtego ambao sasa umetatuliwa.
Kukamilika kwa usajili huo saa chache kabla ya dirisha la usajili kufungwa, kunamaliza mzozo baina mashabiki wa soka nchini ulioibuka kwa baadhi yao kupinga uhalali wa mchezaji huyo kwenda Simba na wengine wakidai alikuwa na uhalali huo.
Soka Awesu Mnyama, Simba, KMC wamalizana
Awesu Mnyama, Simba, KMC wamalizana
Read also