Paris, Ufaransa
Bao pekee la Mallory Swanson limeiwezesha timu ya soka ya Marekani kutoka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Brazil katika mechi ya fainali ya Michezo ya Olimpiki 2024 na kubeba medali ya dhahabu.
Ushindi huo unazidi kumjengea heshima kocha wa Marekani, Emma Hayes kwa namna ambavyo ameiwezesha kutamba katika mashindano yake makubwa ya kwanza tangu akabidhiwe timu hiyo.
Emma, 47, ambaye ni Muingereza alikabidhiwa majukumu ya kuinoa Marekani takriban miezi mitatu iliyopita lakini aliweza kuibadili timu hiyo na hatimaye kuwa tishio hadi kubeba medali ya dhahabu katika Olimpiki.
Bao la Mallory lilipatikana dakika ya 57 baada ya kuinasa pasi ya K Albert na kutibua mtego wa kuotea kabla ya kumtungua kipa wa Brazil, Lorena.
Brazil nao walipambana kusaka bao la kusawazisha na juhudi zao nusura zizae matunda katika dakika 10 za nyongeza baada ya Adriana kuufumania mpira na kuupiga kwa kichwa lakini kipa wa Marekani, Alyssa Nacher alikuwa makini na kuokoa.
Gumzo kubwa katika ushindi wa Marekani ni kocha wao Emma ambaye inadaiwa alishtuka na kutoamini baada ya kutangaziwa nafasi ya kuinoa timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Marekani.
Kwa kipindi kirefu timu ya wanawake ya Marekani ilikuwa tishio kabla ya mambo kuanza kwenda kombo na ndipo uamuzi wa kumkabidhi timu hiyo, Emma ulipofikiwa na hakika hajawaangusha.
Mafanikio ya Emma katika timu ya wanawake ya Chelsea kwa kutwaa mataji 14 katika miaka yake 12 ndiyo yaliyoishawishi Marekani kuamini kuwa ni mtu sahihi kukabidhiwa timu hiyo.
Ushindi wa Marekani pia unamfanya nyota wa muda mrefu wa Brazil, Marta 38 mwenye rekodi za kuvutia na timu hiyo kuiaga kinyonge.
Marta ambaye alitangaza kwamba Michezo ya Olimpiki 2024 itakuwa ya mwisho kwake na timu ya Brazil ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao mengi kwenye fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake na wanaume akiwa na mabao 17.
Kimataifa Marekani yatwaa dhahabu Olimpiki
Marekani yatwaa dhahabu Olimpiki
Read also