Yaounde, Cameroon
Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Issa Hayatou aliyeliongoza shirikisho hilo kwa miaka 29, amefariki dunia jana Alhamisi akiwa na umri wa miaka 77.
Hayatou ambaye anatokea nchini Cameroon, aliingia kwenye uongozi wa Caf mwaka 1988 na kuongoza hadi mwaka 2017 lakini pia aliwahi kushika nafasi kadhaa za juu za uongozi wa Fifa.
Kwa upande wa Fifa, Hayatou aliwahi kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ambayo kwa sasa inajulikana kwa jina la Baraza la Fifa majukumu aliyoyashika kuanzia mwaka 1990 hadi 2017.
Hayatou pia amewahi kuwa rais wa muda wa Fifa kati ya mwaka 2015 na 2016 akishika nafasi ya Sepp Blatter aliyesimamishwa baada ya kuandamwa na kashfa za rushwa na matumizi mabaya ya fedha.
Baada ya kupata habari za kifo cha Hayatou, Rais wa Fifa, Gianni Infantino ametuma salamu za rambirambi akisikitishwa na kifo cha kiongozi huyo ambaye wakati wa ujana wake aliwahi kuwa mwanariadha na pia aliwahi kucheza mpira wa kikapu.
“Nimesikitishwa kusikia habari za kifo cha rais wa zamani wa Caf ambaye pia amewahi kuwa rais wa muda wa Fifa na mjumbe wa baraza la Fifa, Issa Hayatou,” alisema Infantino kupitia mtandao wa Instagram.
Infantino alimtaja Hayatou kuwa ni mtu aliyekuwa na mapenzi katika michezo na aliyejitoa katika maisha yake kwenye uongozi wa michezo.
“Kwa niaba ya Fifa natuma salamu za pole kwa familia, marafiki, jamaa wenzake wa zamani na wote wanaomfahamu, apumzike kwa amani,” alisema Infantino.
Agosti 2021, Hayatou alisimamishwa kwa mwaka mmoja na Fifa kwa kosa la kwenda kinyume na kanuni za maadili baada ya kusaini mkataba mkubwa wa soka mwaka 2016 na kampuni ya habari ya Lagardere ya nchini Ufaransa.
Kimataifa Issa Hayatou afariki dunia
Issa Hayatou afariki dunia
Read also