Columbus, Marekani
Kocha Man City, Pep Guardiola amesema kwamba atakuwa anatumia muda mfupi kuzungumza na wachezaji wake wakati wa mapumziko baada ya timu hiyo kuadhibiwa kwa kuchelewa kuingia uwanjani.
Man City ilikubali kufanya kosa la kuchelewa kuingia uwanjani baada ya mapumziko zaidi ya mara moja bila ya kuwa na sababu ya msingi jambo ambalo ni kinyume kanuni za Ligi Kuu England na hivyo kutozwa faini ya Pauni 2.09 milioni.
Pep ambaye kwa sasa yupo na kikosi cha Man City nchini Marekani kwa ziara ta mechi za kirafiki alisema, “Nimeisoma hiyo habari, nitajitahidi kufanya mazungumzo yangu yawe mafupi wakati wa mapumziko.”
Man City baadaye leo Jumamosi itacheza na Chelsea mjini Columbus ambapo kikosi cha Pep kina wachezaji wachache waliozoeleka kikosi cha kwanza ukiacha baada ya wengi wao kushiriki fainali za Euro 2024 na Copa America.
Katika mechi ya kujipima nguvu Pep amekuwa akimpa nafasi mshambuliaji wake regemeo, Erling Haaland ambaye bado ana matatizo ya hapa na pale ya misuli ingawa kocha huyo alisema kwa sasa hali ya mchezaji huyo si mbaya sana.
Pep pia alikataa kuzungumza lolote kuhusu mshambuliaji Julian Alvarez ambaye kwa sasa yuko na timu ya Argentina kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris ambaye pia zipo habari kwamba Atletico Madrid inamtaka.
Katika hatua nyingine Pep alimpongeza mmoja wa wasaidizi wake, Enzo Maresca ambaye kwa sasa amejiunga na timu ya Chelsea.
Kimataifa Adhabu yampa somo Pep
Adhabu yampa somo Pep
Read also